Saturday, 3 November 2018

JINSI YA KUWAOMBEA WATOTO WAKO,KUANZIA KICHWANI MPAKA MIGUUNI

HOW TO PRAY FOR YOUR CHILDREN FROM HEAD TO TOE.
( JINSI YA KUOMBEA WATOTO WAKO KUANZIA KICHWANI MPAKA MIGUUNI)

Hamjambo Wazazi na Walezi Wenzangu?
Sasa leo ningependa tuhitimishe mada ya WATOTO, kwa kujifunza namna ya kuombea Miili ya Watoto wetu kuanzia kichwani mpaka miguuni. Sio unaomba tu generally kama unaombea chakula, no! Kila kiungo cha mwili wa mtoto wako kina nafasi yake na utendaji kazi wa tofauti.

Yapo mambo KUMI ( 10) Ambayo ningependa tuyaongelee leo:

■Kwanza tuanze na KICHWA
-Unapoombea kichwa chake maana yake unaombea ufahamu wake, yaani akili yake.
Hapa ombea watoto wako waitafute hekima na ufahamu kwa bidii, ili wawe na maarifa ya kupambanua kati ya lililo jema na lile ovu, ili mawazo yao yaelekezwe kwenye kweli ya Mungu.
Text ya kumsomea ni Mithali 2:1-6, inasema hivi, ” MWANANGU, KAMA UKIYAKUBALI MANENO YANGU NA KUYAWEKA AKIBA MAAGIZO YANGU, UKITEGA SIKIO KUSIKILIZA HEKIMA, UKIUELEKEZA MOYO WAKO UPATE UFAHAMU, NDIPO UTAKAPOFAHAMU KUMCHA BWANA NA KUPATA KUMJUA MUNGU. KWA KUWA BWANA HUWAPA WATU HEKIMA NA KINYWANI MWAKE HUTOKA MAARIFA”.

■OMBEA MACHO YAO:
Ombea macho ya mtoto wako. Mungu ayatawale macho yao ili kwamba watazame na kuyaangalia mambo yaliyo mema. Wasitazame visivyofaa. Unajua macho ni mlango mkubwa sana ambao ibilisi huutumia kuingiza kwenye ubongo taarifa mbaya zinazozaa tamaa mbaya. Neno la Mungu linasema, HAWA ALIPOONA LILE TUNDA LINATAMANIKA KWA MACHO AKASHAWISHIKA KULA. MFALME DAUDI ALIPOONA MWANAMKE ANAOGA NAYE ANATAMANISHA, HAKUJALI KUWA NI MKE WA MTU, ALIMCHUKUA AKALALA NAYE. Ndio maana ndugu yetu Ayubu akasema, ” NIMEFANYA AGANO NA MACHO YANGU, BASI NAWEZAJE KUMTAZAMA MWANAMKE? Ni kwamba alijua kabisa, macho yanaweza kuleta shida. Ombea macho ya watoto wako yasitazame vitu visivyofaa.
Text: Mithali 4:25-27
” MACHO YAKO YATAZAME MBELE NA KOPE ZAKO ZITAZAME MBELE SAWASAWA. USIGEUKE KUUME WALA KUSHOTO, ONDOA MGUU WAKO MAOVUNI”.

■ OMBEA MASIKIO YAO
Waombee watoto wako wawe wepesi kusikia. Waelekeze masikio yao kusikiliza maagizo. Wasisikilize taarifa potofu, zinajenga hofu na kutojiamini. Text ni Mithali 8:32-34
” BASI MWANANGU NISIKILIZE SASA, MAANA NI HERI HAO WAZISHIKAO AMRI ZANGU. SIKIENI MAFUNDISHO MPATE HEKIMA, WALA MSIYAKATAE”.
Ombea watoto wako wawe wasikivu, wawe wanakutii, wasikilize maagizo yako ili wasiwe wakaidi.
■ OMBEA VINYWA VYAO
Kama mzazi unatakiwa kuombea vinywa vya watoto wako ili Mungu alinde midomo yao isinene mabaya na wasiwe waongo. Matusi yasitoke kwenye vinywa vya watoto wako. Bali maneno yao yapate kibali mbele za Mungu na yawanufaishe wale wanaowasikiliza.
Text ni Zaburi 34:13,” UUZUIE ULIMI WAKO NA MABAYA NA MIDOMO YAKO ISINENE HILA”.
Halafu mwongoze mtoto wako kukiri maneno haya, ” MAWAZO YA MOYO WANGU NA MANENO YA KINYWA CHANGU, YAPATE KIBALI MBELE ZAKO, EE BWANA MWAMBA WANGU NA MWOKOZI WANGU” Zaburi 19:14.

■ OMBEA MOYO WAKE:
– Mwombe Mungu awape watoto wako moyo wa furaha na kuchangamka. Waombee wamjue Mungu mapema na kumkabidhi Mungu atawale maisha yao. Tusome text ya Mithali 15:13, ” MOYO WA FURAHA HUCHANGAMSHA USO, BALI HUZUNI YA MOYO ROHO HUPONDEKA. MOYO WA MWENYE UFAHAMU HUTAFUTA MAARIFA. BALI KINYWA CHA MPUMBAVU HUNENA UPUMBAVU.
Kwa hiyo moyo wa mtoto wako ukijaa maarifa, kinywa chake hakiwezi kutamka upumbavu. Hutasikia mwanao akitukana.

■OMBEA MIKONO YAO
Ombea mikono ya watoto wako ifanye kazi kwa bidii. Kama ni kusoma basi wasome kwa bidii. Mungu amesema ataibariki kazi ya mikono yako, kwa hiyo kama hana kitu cha kufanya, maana yake Mungu hatakuwa na jinsi ya kumbariki. Waombee wasikae idle. Text: Torati 28:8,” BWANA ATAIAMURU BARAKA IJE JUU YAKO KATIKA GHALA ZAKO, NA MAMBO YOTE UTAKAYOTIA MKONO WAKO KUYAFANYA”.
Kwa hiyo baraka ya Bwana inakuja kwa wale tu wanaotia mikono yao kufanya kazi.

■ OMBEA MIGUU YAO
Ombea watoto wako wasitembee kwenye njia mbaya wala wasiambatane na watu waovu, bali waambatane na wenye hekima nao watakuwa na hekima.
Text: Zaburi 1:1, ” HERI MTU YULE ASIYEKWENDA KATIKA SHAURI LA WASIO HAKI, WALA HAKUSIMAMA BARAZANI PA WENYE MIZAHA”
Hapa sasa ndio vijiweni. Unakuta mtoto anashinda kijiweni anasahau hata kurudi nyumbani kula chakula. Ombea miguu yake.
Wasomee Zaburi 37:23-24, nayo inasema, ” HATUA ZA MTU ZAIMARISHWA NA BWANA. NAYE AJAPOJIKWAA BWANA HUMSHIKA MKONO NA KUMTEGEMEZA”.

■ OMBEA SEHEMU ZAO ZA SIRI:
Hapa sasa usiache kuzungumza nao. Ni marufuku mtu kumshika sehemu hizi nyeti zaidi ya wewe tu mama yake. Mjengee uwezo wa kujilinda na kutoogopa kukueleza iwapo mtu yeyote atamchezea au kumshika sehemu zake za siri. Usiache kumkagua mtoto wako periodically wakati unamwogesha. Kisha waombee watoto wako Mungu awaepushe na zinaa. Atiishe viungo vyao visitumiwe na shetani kufanya zinaa ili wasipate uharibifu. Wasomee neno la Mungu.
1 Wakorinto 6:15-18
” JE! WANANGU, HAMJUI YA KUWA MIILI YENU NI VIUNGO VYA KRISTO? BASI NIVITOE VIUNGO VYA KRISTO NA KUVIFANYA VIUNGO VYA KAHABA? HASHA! IKIMBIENI ZINAA!
Waeleze watoto wako ubaya wa zinaa. Tusiwaonee aibu watoto wetu, aibu haitoki kwa Mungu wazazi, inatoka kwa shetani. Ndio maana baada ya Adamu na Hawa kula tunda walilokatazwa tunaambiwa walijificha kwa sababu WALIONA AIBU. Mbona mwanzoni walikuwa uchi lakini hawakuona aibu? Usikubali kabisa kuona aibu kuongea na watoto wako maswala ya ngono na afya ya uzazi. Usidhani atafufuka bibi yako awafundishe.

■ MWISHO KABISA OMBEA WENZI WAO WA MAISHA.
– Ombea watoto wako sana kwenye eneo hili. Tena omba kweli kweli. Ili Mungu awape wenzi sahihi wa maisha na awakutanishe nao kwa WAKATI SAHIHI. Tunasema Kwa kizungu, ( PRAY THAT GOD MAY LOCATE THEM TO THEIR RIGHT LIFE PARTNERS AT THE RIGHT TIME).
– Neno la Mungu linasema wazi kwamba, ” NYUMBA NA MALI NI URITHI APATAO KWA BABA YAKE; BALI MKE/ MUME ALIYE NA BUSARA MTU HUPEWA NA BWANA. Mithali 19:14.
Kumbe sisi wazazi, tunaweza tu kuwapatia watoto wetu elimu bora, tukawaandalia nyumba za kuja kuishi pamoja na kuwarithisha mali, lakini linapokuja suala la KUOA NA KUOLEWA NI MUNGU PEKE YAKE AWEZAYE KUWAPA WENZI SAHIHI.
– Tunakumbuka Ibrahimu alipokuwa amezeeka sana, akaona asife bila kuacha mwanae Isaka amepata mke sahihi wa kumuoa. Pamoja na kumwandalia Mwanae mali nyingi sana, maandiko yanasema Ibrahimu alikuwa ni tajiri sana wa mifugo fedha na dhahabu, lakini alitambua UMUHIMU wa kupata mwenzi wa maisha aliye sahihi. Na alifahamu kuwa ni mpaka Mungu ahusishwe ndipo mwenza sahihi anapatikana. Tunasoma hivi, NAMI NAKUAPISHA KWA BWANA, MUNGU WA MBINGU NA NCHI KWAMBA HUTAMTWALIA MWANANGU MKE KATIKA BINTI ZA WAKAANANI.BALI ENENDA KATIKA NCHI YANGU NA JAMAA ZANGU UKAMTWALIE MWANANGU MKE. BWANA ATAPELEKA MALAIKA WAKE MBELE YAKO, NAWE UTAMTWALIA MWANANGU MKE KUTOKA HUKO”. Mwanzo 24:1-9.
-Kwa hiyo basi, wazazi na walenzi wenzangu tufahamu hili kwamba WE HAVE A VERY BIG ROLE TO PLAY WHEN IT COMES TO OUR CHILDREN’S MARRIAGE. Nafasi yetu ni kuomba Mungu. Usije huko mbele ya safari ukaanza kumpondea mka mwana wako na kumsumbua, jiulize ULIOMBA? Ni kweli huwezi kumchagulia mwanao mtu wa kumuoa au wa kuolewa naye na wala huwezi kumlazimisha aoe yupi but OMBA ILI MUNGU AMKUTANISHE NA MWENZI SAHIHI. Ndoa ya mtoto wako ikiyumba hata sisi wazazi hatutakuwa na raha.
– Usione mwanao bado mdogo, ukasema akifika chuo kikuu ndio nitaanza kumwombea, infact maombi yako ni AKIBA. Huwezi jua kama bado utakuwa hai ukifikia wakati wao wa kuoa na kuolewa. Anza kuomba sasa hata kama ndio umejifungua jana. Ombaaaa. Mwalimu mmoja alitufundisha akasema, yeye na mume wake, walianza kuombea wenzi wa watoto wao wakiwa na mimba. Yaani as soon as anagundua ni mja mzito, anaanza kuombea mke au mume wa kuoa huyo mtoto. Ataombea wakwe zake, ataombea elimu yake na kazi zake tangu mtoto yuko tumboni. Kwa hiyo akizaliwa mambo yake yanaenda tu kiulainiii kwa sababu wazazi walishaweka akiba ya maombi kwa Mungu.
– Ombea marafiki wa watoto wako.
Mzazi mpendwa, watenge watoto wako na marafiki wabaya kwa njia ya Maombi. Unaweza kugundua watoto wa jirani yako wana matusi au wana michezo mibaya lakini ndio marafiki wakubwa wa watoto wako. Sasa ukitumia nguvu kuwazuia wasiende kucheza huko, hawatakuelewa. Wewe tuma roho ya mafarakano kati ya watoto wako na marafiki wabaya. Unaowajua wewe ni hao tu walioko mtaani, lakini hujui kule shuleni wanaambatana na watoto wa aina gani. Mzungushie mtoto wako ukuta wa moto, uovu usiwakaribie. Wapo wanafunzi wadogo chekechea lakini Wachawi. Naishi Tabata Bima, nilikutana na walimu wa St. Mary’s Orphanage ambayo nadhani sasa haipo tena. Walikuwa wanatusimulia jinsi usiku watoto wanaowafundisha wanavyowawangia. Yaani mtoto ukimwadhibu tu darasani, usiku anakujia kukuwangia live kabisa. Hee! Hiyo hali iliwatesa sana walimu, pakafungwa.
-Pia wapo wanao initiate uchawi darasani kwa watoto wenzao. Nimeoa live mtoto wa darasa la pili anaombewa ana confess kuleta pipi zilizowekwa UCHAWI ili kuwa- initiate watoto wenzake kwenye ulimwengu wa giza waje kuharibikiwa ukubwani.

wazazi wapenzi:
WATOTO NI THAWABU. NI URITHI KUTOKA KWA MUNGU. URITHI HUWA UNATUNZWA ILI UWEZE KUDUMU. WEKEZA KWA WATOTO WAKO. MAFANIKIO YA WATOTO WETU NDIO FAHARI YETU.

Nawasilisha

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...