Saturday, 15 September 2018

Mafundisho ya Askofu Kakobe kuhusu talaka ndoa za Kikristo sio sahihi


Na David Stamen
Makala hii inajibu ile iliyochapishwa katika tovuti hii ya mwanzonews.com ikiwa ni sehemu ya mahubiri ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe iliyokuwa na kichwa kisemacho: Uzinzi haubatilishi ndoa-Askofu Kakobe.
Nianze na nukuu yake kama ilivyoandikwa katika makala hiyo, pale anaposema: KUMWACHA MKE KWA SABABU YA UASHERATI (Mst. 9) Hiki ni kisingizio cha watu wengi wasio na maarifa kuwaacha wake zao. Nyakati za Biblia mtu alipotoa posa kwa mchumba wake, hata kabla hawajaoana, waliitwa mtu na mkewe (KUMBUKUMBU 22:23-24; MATHAYO 1:18-20). Katika uchumba, kama mke huyo alithibitishwa kuwa amefanya uasherati kwa kuwa na mimba au vinginevyo ilikuwa ni halali kumwacha maana ni dhahiri kwamba siyo mwaminifu. Ni kwa sababu hiyo Yusufu alitaka kumwacha Mariamu kwa kudhani alifanya uasherati
.
Vivyo hivyo, katika Kanisa, watu ambao bado ni wachumba, hata kama posa imekwisha kutolewa; mmojawapo anapothibitika kuwa amefanya uasherati, huyo mwenzake ana ruhusa ya kumwacha kwa sababu inadhihirisha kwamba hajaokoka. Lakini mtu na mkewe wakiisha kuoana, uzinzi siyo sababu ya kuwaruhusu kuachana. Mume anapaswa kumsamehe mkewe mara saba mara sabini makosa YOTE kama Mungu katika Kristo alivyotusamehe sisi. Je, tulisamehewa dhambi zote kasoro uzinzi? Jibu ni la! Basi uzinzi siyo kisingizio cha kumwacha mke (WAEFESO 4:32). Mwisho wa kunukuu.
Kuhusu mafundisho yake kuwa uzinzi si sababu ya talaka (kuachana)
Mathayo 19:1-11
Askofu Kakobe anazungumza kuwa uzinzi si sababu ya talaka. Anadai wachumba pekee ndio wanaweza kutengana kama watafanya uzinzi. Anasema wachumba wanatambulika kama wameoana kutokana na maandiko, na hili liko wazi kutoka katika maandiko anayo yanukuu. Anasema pia, Katika uchumba, kama mke huyo alithibitishwa kuwa amefanya uasherati kwa kuwa na mimba au vinginevyo ilikuwa ni halali kumwacha maana ni dhahiri kwamba siyo mwaminifu.
Lakini kifungu anachokinukuu kuthibitisha maneno yake hakitufundishi hivi. Tunapoangalia kifungu hiki kinasema, Pakiwa na kijana aliye mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye; watoeni nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa kuwa hakupiga ukelele, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. (Kumbu.22:23,24).
Hili linaweka wazi kuwa kama mwanamke aliyechumbiwa ataruhusu mwanaume alale naye, ametenda uovu na wote wauawe. Adhabu hii ni sawa kwa wana ndoa pia tunaposoma mstari wa juu yake (Kumb 22:22), na sababu ya adhabu ni sawa, Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli.
Vifungu anavyonukuu Askofu Kakobe, havikutaja kuwa mwanaume aliyemchumbia mwanamke atamuacha kama atafanya uzinzi. Kwanini? hii ni kwa sababu mwanamke kama huyu angeuawa! Tunaona ni jinsi gani Mungu anavyoichukulia kwa uzito hii dhambi, sababu kwa wachumba na wanandoa Mungu si anatoa adhabu ile ile lakini anasema, ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. Ni wazi katika Agano Jipya, katika kanisa la Bwana, hakuna adhabu katika mwili kama hii, lakini tunaona jinsi dhambi hii inavyoharibu maisha ya watu na uhusiano wao na watu wengine.
Katika Mathayo 19 ni dhahiri mazungumzo yalihusu wanandoa tu. Yesu anajibu mstari wa 4-6, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. Hiki kifungu ni zaidi ya sherehe ya ndoa za kisheria au za jumuiya. Ni juu ya kufanywa mmoja, kuwa mwili mmoja, kuhusu kuunganishwa kwa miili katika ndoa.
Tumeona Yesu katika mstari huo wa 4-6 alikuwa akizungumzia wanandoa na si wachumba (wawili hao watakuwa mwili mmoja). Hii ndio maana ya swali la Mafarisayo walilomuuliza katika mstari wa 3. Lilikuwa swali juu ya talaka (kuachana) kwa waliooana na sio kutengana kwa wachumba. Na hili linadhihirishwa na swali la pili la Mafarisayo katika mstari wa 7. Hati ya talaka inayotajwa hapa ni kwa wanandoa, na si wachumba!
Hapa Mafarisayo walikuwa wanasimamia sheria ya Musa katika Kumbukumbu 24:1-4, Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake, kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake. Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine. Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha, na kumpa mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa, aliyemtwaa kuwa mkewe; yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za Bwana; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi.
Hiki kifungu kiko wazi juu ya kupewa talaka na kuolewa tena hakihusu kuchumbiwa na mtu. Tunaona hili kutokana na maneno ya kwanza yaliyotumika hapa, Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa. (Kwa tafsiri ya Biblia ya Kiingereza, When a man has taken a wife and married her.) Hii ni kwa wale waliokwishaoana, kama tunavyoona katika kifungu hiki kizima! Na hiki ndicho kifungu Mafarisayo walichokuwa wanazungumzia! Katika kifungu hiki mwanamke haruhusiwi kumrudia mume wake wa kwanza. Kwanini ? Kwa sababu amekwisha kutiwa unajisi!
Hii inamaana kwamba amekwisha kutiwa unajisi kwa kulala na mwanaume mwingine. Na hili ni muunganiko wa miili uliofanyika katika ndoa zote mbili. Kwa kulala na mwanaume mwingine amefanya jambo ambalo limeharibu uhusiano wake na mwanaume wa kwanza kwa hiyo kumrudia na kulala na huyo mwanaume wa kwanza , ingekua machukizo mbele za Bwana. Kusema kuwa kifungu hiki kinawahusu wachumba ni jambo lisiloelezeka.
Vifungu hivi vinatupa kuelewa muunganiko wa miili una maana kubwa katika Biblia. Ina maana kubwa ya kiroho na tunatakiwa kuelewa hili kama tunataka kuelewa mafundisho ya ndoa na talaka. Paulo anasema, Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. (1 Wakor.6:15-17).
Inashangaza! Haya ni mafunuo kwetu juu ya kweli katika mada hii. Kama watu wawili watalala pamoja kwa njia hii – hata kama ukilala na kahaba- unakuwa mwili mmoja na kahaba! Ukilala na kahaba unafanya mwili wako kuwa kiungo cha kahaba! Watu wawili wanapokutana kimwili ni zaidi ya tunavyofikiri. Mungu ametangaza wawili watakuwa mwili mmoja. Japokuwa hii yaweza kuwa zaidi ya ufahamu wetu, isipokuwa ni ufunuo wa Mungu kwetu juu ya umuhimu wa hili tendo. Maana yake na umuhimu wake ni zaidi ya tendo lenyewe!
Hii ndio maana ya kifungu katika Wakorintho tulichosoma. Kuna kitu zaidi kinatokea kwetu tunapoiungamanisha miili yetu na ya watu wengine! Mungu mwenyewe kupitia neno lake linasema huleta muungano kati ya watu wawili. Ni muunganiko wenye maana kubwa mno-bila kujali tumeoana au la! Kama tulivyoona kwenye hiki kifungu cha Wakorintho! Ndio maana Paulo anasema ikimbieni zinaa,na ndio maana Mungu alisema ni machukizo mwanamke mbele za Bwana mwanamke kumrudia mume wa kwanza akishaolewa na mume wa pili (Kumbu.24:1-4). Hiki kitendo cha mwili kina maana kubwa na pia matokeo na madhara hapa duniani na inawezekana hata ya milele.
Ukweli huu waweza kutusaidia kuelewa kwanini katika Agano la Kale adhabu ya dhambi hii ilikuwa ni ileile kwa waliooana na ambao ni wachumba-waliuawa, hakukuwa na tofauti!
Ndio sababu Yesu alisema pia, Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. (Mathayo 19:9). Hii dhambi ya uzinifu inatengeneza kitu kati ya wawili wanaozini, na kuharibu kitu katika mahusiano ya wanandoa. Ina maana na ni muhimu zaidi ya tendo lenyewe, na tunachoona ina umuhimu kiroho na matokeo ambayo hudhuru uhusiano baina ya mke na mume, katika upendo, imani na uaminifu. Sababu hizi, Bwana Yesu anatoa uzinzi pekee kama sababu halali ya kumtaliki mume au mke wako.
Na huu umekuwa uelewa wa kifungu hiki kwenye Mathayo karibu miaka 2000-na ni kwa sababu nzuri! Kama mume au mke wako akitenda uzinzi uko huru kumwacha. Unaweza kumuacha sababu usinielewe vibaya -alichotenda mwingine (mume au mke wako) ni aina ya talaka, tungeweza sema mbaya zaidi ya talaka kwani talaka ni jambo la hati tu!Na maneno ya Yesu yanathibitisha wazo hili.
Wanafunzi wa Yesu walishangazwa na mafundisho ya Yesu. Na tunaweza kuelewa kwanini pasipo ugumu wowote. Katika desturi yao waliruhusiwa kumuacha, ila sasa Yesu anasema unatakiwa ubaki na mkeo maisha yako yote, isipokua akitenda uzinzi. Kuhusu kukaa na mtu ambaye mwisho wa siku ukajikuta kuna shida au ugumu ni jambo ambalo wanafunzi wake hawakulikubali!
Japokuwa msamaha una sehemu yake, lakini sicho tunachozungumzia hapa! Wala Yesu mwenyewe hakulifanya jambo la msamaha! Hii inatokana na asili ya hii dhambi ya uzinzi na madhara yake! Na Yesu anaruhusu talaka sababu ya asili ya dhambi hii na matokeo yake kwenye ndoa juu ya uhusiano wa mume na mke.
Ipo nafasi ya msamaha, ndiyo! Unapaswa kukabidhi hukumu yote kwa Mungu na kuhakikisha hakuna uchungu, ugumu wa machukizo katika moyo wako juu ya mwenzako. Katika hali hii unaweza kusamehe.Lakini msamaha huu haukufanyi kubakia katika ndoa iliyovunjika sababu ya uzinzi. Hili liliwekwa wazi na Yesu mwenyewe!
Kwa hiyo, kwa mujibu wa mafundisho ya Yesu, mtu anaweza kumuacha mke au mume wake kama ametenda uzinzi. Kama ukiniuliza mimi, lazima waachane mume na mke? sitajadili hili sababu inawakilisha fundisho zima lenyewe. Lakini kufundisha au kuwaambia watu kuwa hawaruhusiwi kuachana (kumpa talaka mume au mke)kama wametenda uzinzi si jambo la Kibiblia kabisa. Zaidi ya kuwa si jambo la kibiblia, fundisho hili linapokubaliwa, linaweza kuwa na matokeo yanayoweza kuharibu au kusambaratisha maisha ya wengi.
Unaweza kuwa katika kifungo katika uhusiano na mtu ambaye ataendelea kuzini kwa sababu unapaswa kusamehe saba mara sabini! Fundisho hili lingekubaliwa, lingeondoa ukubwa wa dhambi hii kutoka kwa wazinzi na mwisho wa siku kuleta fedheha na dharau kwa ndoa za wakristo. (Mimi siwezi kuweka au kutengeneza sheria kwamba ni LAZIMA uachane na mume ua mke wako kama akifanya uzinizi inategemea. Katika somo hili kutokana na maandiko ninaonyesha tu wako huru kumwacha anapofanya dhambi hii.)
Neno la mwisho, japokuwa wachumba wanaotaka kuoana wanatambulika kama wanandoa katika Biblia( kwa maneno mengine, uchumba unakuwa kama alama au ahadi ya ndoa itakayofanyika), hakuna sehemu yoyote katika Biblia wanaitwa kama mume na mke tu. Muktadha na lugha ya kimaandiko huweka wazi kabisa kama kifungu kinazungumzia wachumba, kwa hiyo katika Kumbukumbu inazungumza kuhusu mwanamwali aliyeposwa na mume, kwa hiyo hapa ni dhahiri hawajaoana. Katika Mathayo inasema Mariamu aliposwa na Yusufu kabla hawajakaribiana. Ni sawa na hapa, hakuna mkanganyiko! Maandiko yanapozungumza kuhusu wale ambao ni wachumba huweka wazi,sababu maandiko na maudhui huwa wazi. Hakuna sehemu kwenye Mathayo 19 ambako maudhui au lugha iliyotumika inatufanya tuelewe kuwa inahusu wachumba.Kutoka mwanzo hadi mwisho iko wazi, inahusu watu waliooana. Tena, katika Biblia yote hakuna neno talaka lilipotumika kwa wachumba.
Mwandishi wa makala hii ni mwanatheolojia, mtumishi wa Mungu anayeishi nchini Uingereza. Huja hapa Tanzania kufanya kazi ya Mungu ikiwemo semina na makongamano.

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...