
Bwana Yesu asifiwe…
Imeandikwa ; “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;“Yoh.1:12 ( Andiko letu la msingi kwa leo)
Watu wengi leo wamechanganya maana kamili iliyolengwa/iliyoelezewa katika neno hili la “kupewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu” kama ilivyoelezwa katika Yoh.1:12. Watu wengi wamefasiri isivyo sawa kwamba ukiokoka tu basi unakuwa mwana wa Mungu,au wanasema mtu akimpokea Yesu basi anakuwa mwana wa Mungu.Dhana hii haiko sawa,kwa maana neno halisemi hivyo.
Neno linasema ukimpokea Yesu/ukiokoka unapewa “uwezo” wa kufanyika mtoto wa Mungu. Hivyo ni lazima ujue nini maana ya “kupewa uwezo” pia “kufanyika mtoto kwa kigezo cha kuwa mtoto ni sio mwana”. Neno hili “kupewa uwezo ” lina maana ya kupata nguvu ya kufanyika mtoto wa Mungu kisha ufikie hatua ya tatu ya kuwa mwana. Ni kama vile Ukipewa uwezo wa kuwa mwalimu haina maana ndio mwalimu moja kwa moja saa hiyo hiyo,bali ina maana kuwa uwezo huo utakufanya awe mwalimu. Hivyo basi utagundua kwamba kuna mchakato wa kufanyia kazi “uwezo” ili ufikie hatua ya pili ya kuwa mtoto wa Mungu.
Je hatua ya kufanyika mwana ikoje?
Kwa ufupi;
Kumbuka neno “mtoto” kama lilivyotumika katika Yoh.1:12 halina maana ya neno “mwana“. Mtoto na mwana ni maneno mawili tofauti kabisa. Lugha ya kiswahili imeeleza neno mtoto na imeshindwa kumpa mtu picha kamili kuonesha kwamba ni mtoto wa namna gani anayezungumziwa. Katika biblia ya kiingereza imefauru kuleta tofauti katika neno mtoto na mwana. Katika the Bible in Basic English (BBE),inasema;
“ To all those who did so take him, however, he gave the right of becoming children of God--that is, to those who had faith in his name:” John 1:12
Hivyo neno mtoto limetaja “child” na neno mwana hutajwa kuwa “son”
Hivyo ukisoma tena katika Yohn 1:12 Utagundua ukimpokea Yesu unapewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu ( child of God) lakini ukiendelea katika wokovu hadi kufikia kimo cha Kristo unafanyika mwana wa Mungu ( the son of God). Kufanyika mwana wa Mungu mwana ni mchakato mrefu ndani ya maisha ya wokovu sio jambo la siku moja. Kinachotokea ni kwamba ukimkiri Yesu/ukiokoka unapewa uwezo wa Kiungu kama hatua ya kwanza ya kwenda kufanyika mtoto wa Mungu. Unapozidi kuutunza uwezo huo unaenda kufanyika mtoto hatimaye ukiendelea kukaza kwa Bwana unakwenda kwenye hatua ya mwisho ya kufanyika mwana. Kumbuka;wana wa MUNGU ndio wale wanaoongozwa na Roho mtakatifu (Warumi 8 :14)
Hivyo kuna mafundisho rasmi ya kufanyika “mwana wa Mungu” kama hatua ya juu sana katika wokovu. Katika hatua hii mtu uongozwa na Roho mtakatifu,akiisikia sauti yake na kuyafanya yale tu Roho ayasemayo. Uwana haufanywi kwa kumkiri Kristo Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wako kwa siku moja,bali uwana ni mchakato mrefu katika maisha ya wokovu baada ya kumkiri Yesu awe Bwana na Mwokozi wako.
Ni mtoto ndie anaekwenda kufanyika mwana.
Katika hali ya kawaida,mtoto anapozaliwa hutegemewa kukua. Zipo hatua za msingi za ukuaji wa mtoto hata kufikia utu uzima. Mojawapo ya hatua ya msingi ni kuhakikisha anakula mlo kamili ikiwemo maziwa ya mama yake ambayo kawaida hayajachakachuliwa (1 Petro 2:2). Mtoto yoyote asipopata mlo kamili upatwa na koshakoo na hatimaye hudhoofu hata kuvamiwa na magonjwa mbali mbali. Katika hali hiyo hiyo,mtu anapookoka anazaliwa mara ya pili,hivyo anafanyika mtoto mchanga anayestahili apate mlo kamili wa kiroho ambao ni neno sahihi la Kristo lisolochakachuliwa.
Akiendelea kudumu katika kula vizuri kiroho na kupata maongozi mbali mbali ya ukuaji wake,hatimaye mtoto atakuwa vizuri hata kufikia utu uzima aliyekomaa,mwenye kuweza kuisikia sauti ya Baba yake. Hatua hiyo huitwa “uwana” . Hivyo kufanyika “mwana” ni hatua ya kumlingana Mungu alivyo. Ni kiwango cha juu cha ukuaji wako wa kiroho hatimaye kuongozwa na Roho mtakatifu mwenyewe (Warumi 8:14). Mfano mzuri,ni Yesu ambaye aliitwa mwana-wa Mungu,huyu Yesu hakufanya jambo lolote kwa matakwa yake bali Roho wa Mungu ndiye alimuongoza kuyafanya yote katika yote.
Hivyo utagundua ipo kazi kubwa ufikie nafasi ya “uwana” si lelemama!!! Wala si mchezo!!! Kuna kazi ya kujidhabihu kweli kweli,kwa kuyafisha matakwa yako,bali Bwana akaweke mapenzi yake..
Ni makosa kutafsiri ( Yoh.1:12) kwamba ukimpokea Yesu basi wewe ni mwana wa Mungu. Kwa ufahamu huu,sasa yafaa umueleze mtu ukweli kwamba kufanyika mwana wa Mungu ni mchakato wa juu,ila ukimpokea Yesu unafanyika mtoto wa Mungu ( child not son) kama ukiendelea hapo,kisha kuna kazi ya kufanyika mwana wa Mungu (son).
No comments:
Post a Comment