Tuesday, 17 July 2018

UNYENYEKEVU NI GHARAMA

“Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” #Marko 10:35-45
Nakusalimu mwana wa Mungu katika jina la Yesu.
Ninamtukuza Mungu kunipa neema ya kumtumikia siku njema ya jumatano ya leo. Nikuombe tu mteule usiache kunitegemeza katika maombi kila upatapo nafasi. Kwamba neema ya Mungu izidi kunifunika katika kuitenda kazi yake. Wakati mwingine si rahisi sana kuelewa vita ambavyo watumishi wa Mungu wanapitia kwa sababu tu unawaona wanatembea katika neema ya Mungu. Lakini hebu tenga muda kidogo kuwaombea watumishi wa Mungu. Niombee pia upatapo nafasi.
Mwana wa Mungu unyenyekevu ni kitu chenye gharama kubwa sana katika maisha. Kinyume cha Unyenyekevu ni KIBURI/KUJIINUA!! Hutanielewa kama Mungu hajakuweka kwenye nafasi fulani kwenye maisha yako. Lakini kama Mungu amekuweka kwenye nafasi fulani utaelewa jinsi Shetani ambavyo huwa anawajaribu wanadamu kwa kujiinua. Mungu akikuweka kuwa na nafasi ya fedha na mali, Mungu akikuweka kuwa msomi, Mungu akikupa neema ya karama na huduma fulani, Mungu akikupa neema ya kuwa mwenye mamlaka au mtawala, Mungu akikupa vitu fulani ambavyo wengine hawana angalia sana mwenendo wa maisha yako ipasavyo.
Huwa ninapenda kufanya tathmini jinsi ambavyo roho ya kujiinua inavyosumbua watu kwenye maeneo mbalimbali. Huwa naona roho ya kujiinua inavyotusumbua watumishi wa Mungu. Huwa ninaiona roho ya kujiinua inavyowasumbua wafanyabiashara, huwa naiona roho ya kujiinua inavyowasumbua wafanyakazi, huwa naona roho ya kujiinua inavyowasumbua wanasiasa na watawala kwa ujumla.
Ndugu lazima tujifunze kuipinga roho ya kujiinua ndani yetu. Mtume Paulo alipata kukemea watu roho ya kujiinua kwa sababu tu walijiona wana akili sana. “Msiwe watu wa kujivunia akili” #Warumi 12:16.
Mtume Petro akizungumza na vijana kwa mapana zaidi akakemea roho ya kujiinua akisema ‘Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema’ #1Petro 5:5
Kiburi kikiinuka katikati ya watakatifu hatutaweza kuhudumiana kama BWANA atakavyo. Huyu akijiona ni mkuu kuliko yule hatakuwa na utayari wa kumhudumia huyo anayemuona ni mnyonge. Katika Kanisa watu wakijiona wenyewe ni wa thamani sana kwa kuwa tu wamekirimiwa karama fulani na wengine hawajakirimiwa karama walizo nazo wao; hawatakuwa na utayari wa kuwahudumia wengine. Mungu amegawa vitu, amegawa karama na huduma ndani ya Kanisa ili tuweze kuhudumiana. Hajatupa huduma na karama kwa ajili yetu na familia zetu bali amezitoa kwa ajili ya Kanisa lake mwenyewe.
Jumatano hii mpendwa wangu hebu ungana nami kuomba neema ya unyenyekevu ndani yetu. “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake” #Wafilipi 2:3
Huwa napenda kumwomba Bwana anitengeneze, anifinyange kwa upya kila siku akiondoa moyo wa kiburi ndani yangu. Akiondoa moyo wa jiwe na kuniwekea moyo wa nyama ili niweze kumtumikia pasipo majivuno tena kwa unyenyekevu mkuu. “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” #Ezekiel 36:26. Maandiko yanatushauri tujifunze kuwa wanyenyekevu kama Bwana Yesu alivyokuwa mnyenyekevu. Tusijivune kwa sababu ya vile Bwana ametupa.
“Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.” #Wafilipi 2:5-11
Tukijifunza kuwa wanyenyekevu basi Mungu atatuinua tu. Roho Mtakatifu asema “Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua” #Yakobo 4:10
Mwenye masikio na asikie na Mungu aliye hai akubariki.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nawe mwana wa Mungu na ikiwa umebarikiwa basi share ujumbe huu kwa mwingine naye abarikiwe
“YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, YAWEZEKANA KWA MUNGU” #LUKA 18:27

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...