Saturday, 28 July 2018

HUDUMA TANO TEULE.

HUDUMA TANO TEULE.

Image result for huduma tano za kanisa
*WAEFESO 4: 11 – 14.*
*11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
 Image result for huduma tano za kanisa
Katika maandiko yote katika bibilia ambayo yanazungumzia huduma ambazo Mungu kupitia Yesu Kristo amezitoa na kuziweka ndani ya Kanisa, hili ni andiko la pekee ambalo linataja huduma zote tano na majukumu yake ya ujumla ndani ya mwili wa Yesu Kristo.
Sasa yapo maandiko mengine mengi ambayo yanataja huduma mojawapo au baadhi ya hizo ambazo zimetajwa kwenye hili andiko lakini hili andiko ambalo tumenukuu ndo andiko la pekee ambalo zote zimetajwa kwa pamoja alafu majukumu yake ya jumla kwa pamoja yakaainishwa hapa.
Ili kuweza kujua kama mtu anayedai kuwa yeye ni huduma fulani, pamoja na kujua mambo muhususi yanayohusu hiyo huduma kama ambavyo yameainishwa katika maandiko sehemu nyingine katika bibilia ni muhimu sana ujue haya majukumu ya jumla ya huduma zote na kama katika utendaji wake pamoja na hivyo vya kipekee kwa huduma husika anayodai yeye ni, lazima hizi hapa zilizotajwa awe anafanya kwa kushirikiana na huduma hizo zingine.
Maandiko yanatuambia kuwa alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu.
Hii sentensi ilivyokaa imepelekea wengine kusema kuwa zipo huduma nne na mimi sitofautiane nao sana.
Ni kweli sentensi ilivyokaa inaonyesha wazi kabisa kuwa kuna huduma zifuatazo:
*1. Mitume.*
*2. Manabii.*
*3. Wainjilisti.*
*4.Wachungaji na Waalimu.*
Katika pita pita yangu nimeona wachungaji wasio waalimu na nimekutana pia na waalimu wasiyo wachungaji na imenipelekea kuamini kuwa zipo tano.
Lakini pia wale wanaosema zipo nne hawajakosea pia kutokana na mantiki ya jinsi hiyo sentensi ilivyotungwa.
Sasa maandiko yanaanza kuainisha majukumu ya jumla na ya pamoja ya hizi huduma (ziwe tano au nne haina shida kabisa).
*i).* Hizi huduma kwa pamoja zinawakamilisha watakatifu hata kazi ya huduma itendeke.
Kuna tafsiri zingine zinasema kuwa zinawaandaa watakatifu kwa ajili ya kufanya kjazi ya huduma.
Kuna tafsiri ambazo zinasema kuwa zinaweka mikononi mwa watakatifu vitendea kazi ili kazi ya huduma itendeke.
Wito wa kuifanya huduma sio kwa ajili ya watu wachache waliyo na mmojwapo ya hizi huduma ambazo zimetajwa.
Wito wa kufanya huduma ni kwa ajili ya kila mmoja wetu aliyeokoka.
Lakini wenye jukumu la kutuandaa Kanisa la Yesu Kristo kwa ajili ya kufanya hizi kazi za huduma ni hawa wandugu waliyoitwa kwenye hizi ofisi teule.
Kwa hiyo kama mtu ni mtume, au nabii, au mwinjilisti, au mchunagaji au mwalimu, pamoja na majukumu ya kipekee yanayoendana na ofisi yake lakini lazima atahusika katika kuwakamilisha watakatifu, kuwaandaa watakatifu, na kuweka mikononi mwao vitendea kazi ili kazi ya huduma itendeke.
Sio tu watawakamilisha watakatifu, kuwaandaa na kuweka mikononi mwao vitendea kazi kwa ajili ya kufanya kazi ya huduma lakini pia ili mwili wa Kristo ujengwe.
Moja ya vitu ambavyo vinaweza vikaanza kuleta mashaka katika madai ya kuwa fulani ni mmojawapo ya huduma hizi teule ni ile yeye kujenga Ufalme wake badala kujenga mwili wa Kristo.
Hili jukumu ambalo tumepewa kujenga mwili wa Kristo unatoa uhuru kwa yeyeote kati ya hawa ambao wapo kwenye huduma hizi teule kuyasemea mambo ambayo anaona ni hatari kwa ujenzi, ufanisi, mafanikio na ustawi wa mwili wa Kristo.
Tukumbuke kuwa Kanisa sio la mtu awaye yeyote.
Kanisa ni la Yesu Kristo na kama kuna kitu hakijakaa sawa anaweza akamgusa mtu kuyasemea hayo kwa niaba yake.
Kumbuka Yesu alisema alipokuwa akiongea na Petro kuwa Yeye atalijenga Kanisa Lake na milango ya kuzimu haitalishinda.
Hata Paulo Mtume alithubutu kusema kuwa Yeye ni mjenzi stadi mwenye hekima na akadai kuwa ameuweka msingi lakini kila ajengaye juu awe makini sana anajengaje na anajenga kwa kutumia nini.
*ii).* Jukumu lingine la hizi huduma kwa pamoja na kwa ujumla kama zilivyoainishwa na mistari ambayo tumetoka kuinukuu ni kulileta Kanisa katika umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUngu.
Dini na madhehebu haziwezi kutufikisha hapo.
Ni hizi huduma teule kwa kusimama kwenye nafasi zao kama walivyotolewa na Kristo.
Hizi huduma zinapotekeleza majukumu yao zitauleta mwili katika umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu.
Kama Kanisa halikui katika kumfahamu sana Mwana wa Mungu na halikui katika umoja wa imani basi hizi huduma teule hazitekelezi wajibu wao ipasavyo.
Kama ni kakundi fulani tu kanajiona kenyewe kako bora kuliko sehemu nyingine ya mwili wa Kristo basi hiyo ni hali iliyo kinyume na dhumuni la kuuleta Mwili wa Kristo katika umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu.
Leo hii tumetengana sana kiimani.
Huyu anaamini hiki, yule kile.
Hii ni kwa sababu hatujafanya maandiko ndo msingi wa kuamini kwetu wote.
Mbaya zaidi yapo makundi ambao wanaamini vitu visivyo na mashiko katika maandiko.
Na hii imesababishwa na watu wanaodai kuwa wao ni mojawapo ya huduma hizi teule.
Hawa watiu wanadai kuwa Mungu aliwatokea na kuzungumza nao na kuwafunulia lakini hicho wanachodai kuwa Mungu aliwatokea na kuwafunulia kinakinzana na maandiko, na wakichanganyamo na tu muujiza uchwara na twa uongo viwili vitatu watu wanawaamini alafu kanazaliwa kakundi ambako kenyewe hakana ushirikiano na sehemu iliyosalia ya mwili.
Hii ni kinyume kabisa na jukumu hili ambalo tumelianisha la kuleta Kanisa katika umoja wa imani.
Leo hii watu wanawajua, kuwasikiliza, kuwaamini, kuwatii na hata kuwataja wale wanaodai wao ni mojawapo ya huduma teule kuliko hata Yesu.
Kama tukiwa huduma teule tutaelekeza watu katika kumjua sana Mwana wa Mungu.
*iii).* Hizi huduma teule zitashirikiana kuleleta kanisa kuwa mtu mkamilifu na tena kwenye cheo cha utimilifu cha Kristo.
Ili hili liwezekane lazima hizi huduma pamoja na majukumu mengine ambayo ni ya kipekee kwa huduma hiyo, zifundishe maana maarifa yanakuza na kumfanya mtu azidi kuwa mkamilifu.
Katika utekelezaji wa haya majukumu ni ili Kanisa lisiendelee kuwa watoto wachanga wanaotupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu ambazo kimsingi ni kwa hila za watu na ujanja huku tukifuata njia za udanganyifu.
Kuna watu wengi sana ambao wanajiita watumishi ambao kimsingi ni watu wa hila tu, wajanja wajanja ambao wanadanganya watu.
Namna mojawapo ya kuwatambua ni je wanafanya haya yaliyoainishwa na hili andiko tulilonukuu?

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...