Wednesday, 7 November 2018

MAOMBI YA KUFUNGA.

mch.Madumla
Na Mch.G

Bwana Yesu asifiwe…
Mojawawapo ya mafundisho mazuri na yenye nguvu ni mafundisho yanayohusu maombi ya kufunga. Yafaa kila mwamini awe mwombaji mzuri na mfungaji mzuri,lakini mambo haya hayawezekani kama hujafundishwa na kuelewa. Uombaji na kufunga ni roho kamili inayokaa ndani ya mwamini. Hivyo basi kupitia fundisho letu siku ya leo,hatuna budi kuligawa katika vipengele vinane. Tutajifunza kwa ufupi juu ya vipengele hivi,kama ifuatavyo;
  1. Nini maana ya kufunga.?
  2. Kwa nini tunafunga?
  3. Chanzo cha maombi ya kufunga.
  4. Aina za maombi ya kufunga.
  5. Mifano ya watu waliofunga na wakafanikiwa.
  6. Nini faida ya maombi ya kufunga?
  7. Hasara ya kuishi bila maombi ya kufunga.
  8. Ninawezaje kufunga/ ninawezaje kuishi maisha ya kufunga.?

01. NI NINI MAANA YA KUFUNGA?
Kwa mujibu wa biblia,zifuatazo ni tafsiri mbili za neno kufunga;
01.Kufunga ni hali ya kuunyima mwili chakula,vinywaji,na starehe  kwa muda fulani uliotengwa. Tena ni hali ya kuutesa mwili katika kawaida yake kwa ajili ya Mungu.
“Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga,Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta.”Zaburi 109:24. Pia Zab.35:13c “… Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga;…”
Katika maandiko hayo mawili tunaona yanatueleza jinsi mwili ulivyodhoofika kwa sababu ya kufunga. Tunapoona ya kuwa mwili umedhoofika,basi tunajua ya kwamba mwili huo ulinyimwa chakula pamoja na starehe. Kumbuka;Kila mwili wa mtu unapenda kula vizuri,kunywa vizuri na pamoja na starehe fulani hivi. Mwili haupendi masumbufu yakunyimwa mahitaji yake,sasa katika kufunga mwili unanyimwa vyote hivyo.
Starehe mojawapo ambayo mwili unapenda ni kulilaksi katika piga story. Mfano mara nyingi utaona watu wakitoka huku hadi kule kwa ajili ya kupiga soga tu. Mwingine anatoka tabata mpaka mbezi beach kwenda kwa rafiki yake ili apige story tu,kisha anarejea kwake. Kwa habari ya kufunga,starehe nazo zinafungwa hata hizo za kwenda kuzurula zurula kwa ajili ya stori,bali afungaye anapaswa awe na muda mwingi katika kuomba na si vinginevyo.
02. Kufunga ni tendo la imani la kuusulubisha mwili katika matamanio yake yote,na kuihuisha roho kwa njia ya maombi. Ni dhahili kabisa kwamba kila afungaye ni lazima kwanza awe na imani kwa kile akiombacho. Tendo la kufunga ni la kiimani zaidi,ndio maana leo kuna watu waliokosa imani hii ya kufunga na wameshindwa kufunga.
02.KWA NINI TUNAFUNGA?
Zipo sababu nyingi zinazotupelekea tufunge,lakini kati ya sababu hizo ifuatayo ni sababu kubwa nayo ni;
▪Tunafunga kwa sababu kufunga ni mojawapo ya nguzo kubwa ya imani yetu katika Kristo Yesu. Neno hili “ nguzo ya imani” ina maana “ uimara wa imani yetu ” . Tuangalie hili sawa sawa na neno liliohubiriwa na Yesu. Ikumbukwe kwamba mkazo wa ujumbe wa Yesu Kristo kwa kila mwamini ni kuishi maisha ya kufunga na kuomba. Yaani suala la kufunga na kuomba liwe ni mchakato wa maisha yetu ya kiimani. Anasema ; “ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]” Mathayo 17:21
Tafsiri halisi ya andiko hili ni kufunga na kuomba kama mchakato mzima wa maisha ya mwanadamu. Hapa hapana maana kwamba ufunge kwa mambo magumu tu,bali ufunge mara kwa mara kwa sababu ni moja ya msingi wa imani yetu. Neno la Mungu linatutaka tuwe na maombi na mfungo endelevu kama nguzo/msingi wa imani yetu.  Haya mawili “kufunga” na “kuomba” yanakwenda pamoja,ni mapacha.
Kwa maana mtu mwombaji anapaswa awe mfungaji. Yeye aombaye mara kwa mara bila kufunga hapokei majibu yote kwa maana ameacha kufunga kama utaratibu tena mengine hayatoki namna hii bila kufunga nakuomba. Naye vivyo hivyo yeye afungaye pasipo maombi basi funga yake hukosa nguvu kwa sababu hakuomba wakati wa kufunga.
03. CHANZO CHA KUFUNGA.
Hapo zamani maombi ya kufunga ilikuwa ni njia ya siri ya kupata jawabu juu ya  jambo fulani gumu lisilokuwa la kawaida. Kwa sababu ilikuwa ni siri kwa waaminio,hivyo haikufanywa mara kwa mara. Waamini wa kwanza waligundua kufunga kama njia ya kujibiwa na Mungu katika mambo yao magumu wasiyoyaweza. Watu walikuwa wakiomba na kufunga kama sehemu ya kumlilia Mungu.  Mfano tunaweza tukauona pale wana wa Yuda chini ya mfalme wao Yehoshafati walipoinukiwa na mataifa matatu yenye nguvu,waliinukiwa na wana wa Moabu,na wana wa Amoni na wana wa Wameuni. Lakini Yehoshafati akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote ( 2 Nyakati 20:1-3).
Na mwishoe akina Yehoshafati wakaibuka washindi. Lakini ukichunguza kilichowafanya waibuke washindi wa vita ni ile hali ya kumtafuta Bwana Mungu kwa njia ya kufunga na kuomba.
Katika agano jipya,Yesu anakuja na kutuambia ya kwamba sisi sote tujifunze kwake ( Mathayo 11:28-30) . Tunapojifunza kwa Yesu,tunajifunza pia maisha ya kuomba na kufunga. Hii ina maana kufunga ni njia ya Mungu ya kutufanya sisi tunaomtafuta Yeye tumuone wakati tumeisurubisha/tumeitesa miili yetu.Kwakuwa Mungu ni Roho nasi imetupasa kuwa watu wa rohoni kila wakati. Na kufunga ni mojawapo ya mazoezi ya utauwa ya kuwa rohoni.
04.AINA ZA MAOMBI YA KUFUNGA.
Kwa mujibu wa imani yetu sisi tuliookoka,tuna aina tatu za funga ya kweli. Nazo ni;
i)Kufunga kwa nusu siku.
Funga hii ni funga ya kawaida tuliyoizoea wengi. Ni pale ambapo mwombaji hujijima chakula kwa masaa 12 ya siku,yaani kuanzia asubuhi hadi jioni saa 12 jioni kisha unafungulia kwa chakula. Ndani ya masaa hayo ya nusu siku hupaswi kula wala kunywa wala kuzurula zurula bali kutulia srhemu moja ya maombi hukiwa umefunga. Biblia inamtaja Ana binti Fanueli nabii mke aliyekuwa akifunga mara kwa mar,haondoki hekaluni ila kusali na kufunga ( Luka 2:36-37)
ii) Mfungo wa tatu kavu.
Ni mfungo wa kutokula wala kunywa muda wa siku tatu. Dhima kubwa ya mfungo wa namna hii ni kwa ajili ya mambo makuvwa magumu yasiyowezekana katika hali ya kawaida. Mfano tunasoma;“ Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.” Esta 4:16
Hiyo ni habari ya Esta mwanamke shujaa aliyeingia kwa mfalme kinyume cha utaratibu. Kwa sababu kulikuwako na amri ya kuwaangamiza Wayahudi wote,naye Esta akaenda kwa mfamle kama njia ya kubatilisha hukumu ya maangamizo yao.
Paulo mtume naye alifungishwa na Bwana muda wa siku 3 kavu Biblia inasema ;“Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.” Matendo 9:9. Katika mifano hiyo miwili,inatupa picha jinsi mifungo ya tatu kavu yalikuwa yakifanywa kwa sababu ya kuwepo kwa jambo kubwa zito.
III) Mfungo wa kavu kwa neema.
Mfungo wa kavu kwa neema ni mfungo unaotolewa kwa neema kubwa sana na kwa watu wachache. Mfano Yesu aliwezeshwa na Bwana kuingia katika mfungo wa namna hii bila kula wala kunywa muda wa siku arobaini ,imeandikwa “ Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.” Mathayo 4:2
Musa naye aliwezeshwa na Mungu kufunga kwa neema siku arobaini bila kunywa wala kula ,imeandikwa ;“ Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.” Kutoka 34:28
Vile vile Eliya naye akatembea katika mfungo siku arobain ;“ Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.” 1 Wafalme 19:8
Kumbuka;
Isaya 58:6-8 Inaeleza aina fulani ya mfungo ambao umetajwa kwa jina la swaumu. Mfungo huu umetajwa kama mfungo lakini ni maisha ambayo Bwana Mungu anatutaka tuweze kuishi,maisha hayo ni maisha ya kujitoa kwa wengine ni sawa na mfungo maana unajinyima wewe na kumgawia mwingine mwihitaji.
05.MIFANO YA WATU WALIOFUNGA WAKAFANIKIWA.
Wa kwanza ni Yesu mwenyewe Yeye ambae ndio kielelecho chetu. Yeye ingawa alikuwa Mungu lakinialipoonekana sawa na mwanadamu aliishi maisga ya maombi kila wakati na kufunga. Wengine wachache ni kama ifuatavyo;
  1. Esta. – Esta 4:16
  2. Musa -Kutoka 34:28
  3. Eliya mtishbi-1 Wafalme 19:8
  4. Hana mama yake Samweli. 1 Samweli 1:18
  5. Ana binti fanueli – Luka 2:36-37
  6. Danieli – Danieli 9:3,10:3
  7. Nehemia- Nehemia 1:4
  8. Watu wa Ninawi -Yona 3:5
  9. Paulo mtue –  2 Wakorintho 11:27
  10. Kanisa la kwanza huko Antiokia – Matendo 13:2-3
06.FAIDA YA MAOMBI YA KUFUNGA.
  1. Kukujengea misuri ya imani
  2. Kuvikwa nguvu za kiroho.
  3. Kuvikwa sila zote za Mungu kwa ajili ya kuzipinga hila zote za shetani.
  4. Ni chanzo cha kupata kuona kiroho.
07.HASARA YA KUISHI BILA KUFUNGA.
Moja katika ya hasara kubwa ya kuishi bila kufunga ni kukosa nguvu rohoni.
08. NINAWEZAJE KUISHI MAISHA YA KUFUNGA.
Ninakupa njia moja tu iliyo kubwa itakayokuwezesha uwe na maisha haya ya kufunga na kuomba,nayo ni; -.Anza mazoezi ya kufunga kidogo kidogo kila wakati fulani hivi labda kila mwezi. Na kila ufungapo ni lazima uwena sababu nzuri inayokufany ufunge,yaani ni lazima ufunge na uwe na neno litakalosimamia nia yako ya kufunga.

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...