Thursday, 4 October 2018
VIFUNGU VYENYE UTATA - WANAWAKE KUZUILIWA KUNENA NDANI YA KANISA
"Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo.
Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa"
#1Kor. 14:34,35
Nakusalimu mpendwa wangu katika jina la Yesu. Namtukuza Mungu kutukirimia neema ya uzima katika siku njema ya leo kwamba tukamtumikie kwa nguvu zetu zote. Nilikuahidi kugusia vipengele kadha wa kadha vyenye matatizo vikiwazuia wanawake kutenda kazi ya Mungu kinyume na agizo la Mungu kama alivyowaumba mwanamke na mwanaume. Leo tunapoenda kufunga na kuomba kuutafuta uso wa Mungu naomba uungane pamoja nami.
Kifungu ambacho nimekinukuu hapo juu kimetumika vibaya sana na wanaume kuwanyamazisha wanawake Kanisani na haya kwenye nyanja mbalimbali za maisha.
Kama kweli Mtume Paulo alikuwa amekusudia maneno haya iwe amri ya kuwanyamazisha wanawake basi inapingana na ukweli ambao yeye mwenyewe ameusema katika waraka wake huo huo. Katika waraka huo huo wa Paulo sura ya 11 Paulo anafundisha jinsi wanawake ambavyo wanaweza kushiriki katika huduma ndani ya Kanisa katika kutoa unabii na katika kuomba.
Paulo kama angekuwa amekusudia kunyamazisha na kufanya wanawake kuwa viziwi na mabubu ndani ya Kanisa angekuwa wa ajabu sana. Kuna umuhimu wa kuyachunguza maandiko haya kwa kina. Kuna umuhimu wa kuyachunguza maandiko tokea kwenye asili yalivyoandikwa. Nataka tuyachunguze maneno haya matatu:
1. Wanawake.
Neno wanawake lililotumika hapa ni neno la kiyunani 'gune' ambalo humaanisha mke (sio mwanamke yeyote bali aliyeolewa). Maana yake nini? Ujumbe huu uliwahusu zaidi wanawake walio katika ndoa.
2. Kunena
Neno 'kunena' kama lilivyotumika hapa kwa kiyunani ni 'laleo' lenye maana ya kutoa hotuba ya maneno ya ukelele hovyo hovyo. Kumwita mtu kwa majivuno bila adabu na heshima kwa wengine.
3. Inenavyo
Kinyume na laleo, neno 'inenavyo' lilivyotumika hapa kwa kiyunani ni 'lego' likimaanisha 'kunena wazo au mafundisho kwa utaratibu'.
Tafsiri halisi ambayo ingeweza kunenwa hapa ingesomeka hivi kwa ajili ya mstari wetu hapo juu:
"Wake wajiepushe kutoa maneno yenye ukelele wakikatiza mikutano ya kanisa wakikatiza kwa maneno ya hovyo hovyo ya ukelele yakijaa majivuno ya kiburi au kuwaita wengine kwa njia ambayo haina adabu au heshima katika Kanisa. Lakini wanaagizwa kuwa na utii kama sheria isemavyo. Na kama wanataka kuuliza chochote wawaulize waume zao huko majumbani mwao kwani aibu kwa wanawake kunena kwa aina hiyo ndani ya Kanisa"
Sio rahisi sana kuelewa ujumbe huu Paulo alikuwa akiwaeleza namna ya kuwa na adabu kanisa la Korintho kama huna uzoefu wa huduma. Ndugu kuna maeneo unaweza kwenda kuhudumu watu hawana utaratibu kabisa kuwa na adabu wawapo ibadani.
Mahali fulani nilienda kuhudumu watu wanapokea simu wakiwa ibadani. Tena simu zikiwa na sauti. Kituko mahali fulani kilitokea nilimuona mtu akiongoza ibada na katikati akiwa madhabahuni simu ikaita kwa sauti akapokea akamwambia "niko ibadani"!!. Mazingira kama haya usipoweka utaratibu hamtakuwa na ibada.
Kanisa la Korintho lilikuwa na tabia za ajabu sana ambazo zilimgharimu Paulo kufanya matengenezo. Ni katila kanisa hili hili watu walikuwa wakienda ibadani na njaa na kula mkate na divai hadi wanalewa! Hata Paulo akawauliza hamna maeneo ya kwenda kulewa hadi mje kanisani?
Kwa hyo jamii ya wakorintho ilikuwa na shida sana. Inaonekana kana kwamba wanawake hawakuwa na adabu ndani ya ibada. Lakini kiukweli Paulo hakuwa akiwafunga mdomo wanawake.
Kesho tutaangalia kifungu kingine kinacholeta shida cha Wanawake kutokufundisha kanisani.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu uwe pamoja nawe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...
-
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...
-
Bwana Yesu asifiwe… Imeandikwa ; “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; “Y...
-
Ni miaka mingi nimekuwa nikijiuliza swali hili, nitawezaje kumpenda Mungu kwa moyo wangu wote, kwa akili zangu zote na kwa nguvu zangu zote...

No comments:
Post a Comment