Saturday, 6 October 2018

UMEOTA NDOTO GANI LEO?



Ukiota ndoto alafu huko kwenye ndoto ukaona vitu visivyo sawa na mapenzi ya Mungu acha kuogopa na kuanza kuwehuka kwa sababu ya ndoto uliyoota.

Nakubali kuwa ndoto ni halisi na ni moja ya njia ambazo shetani anatumia kushambulia watu kwenye ulimwengu wa roho.

Pia nakubali kuwa kama ambavyo Mungu anaweza kuzungumza na mtu kupitia ndoto na kupanda ndani yake imani kadhalika shetani anaweza kuzungumza na mtu kwenye ndoto na kupanda hofu.

Kanuni za hofu na imani ni zile zile.

Imani ni kuwa na uhakika wa jambo unalolitarajia na kadhalika hofu ni kuwa na uhakika wa jambo unalotarajia.

Unachoamini kinatokeaga kadhalika unachoogopa kinatokeaga.

Imani huleta mema ya Mungu maishani mwetu kadhalika hofu huleta mabaya ya shetani maishani mwetu.

Imani inahudumu uzima katika maisha ya mtu na kadhalika hofu inahudumu mauti katika maisha ya mtu.

Ndoto za kiMungu huachilia mapando ya kiMungu katika maisha yetu kadhalika ndoto za kishetani huachilia mapando ya kishetani maishani mwetu.

Pamoja na kweli zote hizi lakini kumbuka tu kuwa hakuna silaha itakayofanyika dhiki yako itakayofanikiwa.

Kwa hiyo hata shetani arushe silaha kinyume nawe katika ndoto jua, amini na tamka kuwa haitafanikiwa.

Kitu kingine cha kutambua ni kwamba pamoja na kwamba wewe umelala lakini Yeye akulindaye hasinzii wala halali kwa hiyo atakulinda na kila shambulio dhidi yako unapokuwa umelala.

Alafu Yeye atawafanya hao adui wainukao kinyume nawe waanguke mbele yako.

Watakutokea kwa njia moja ila Bwana atawasambaratisha kwa njia saba.

Alafu hutaogopa hofu ya ghafla wala mshale urukao gizani.

Kila mshale ambao shetani anaurusha kinyume nawe gizani, usiku, kwenye ndoto Mungu ni ngao yako na kigao chako.

Acha kuogopa kile adui anaweza kufanya dhidi yako katika ulimwengu wa ndoto maana ni nani asemaye neno nalo likawa ikiwa Bwana hakuliagiza.

Tena yamkini watakusanyana ndidi yako lakini sio kwa shauri la Bwana.

Wowote watakaojikusanya juu yako wataanguka kwa ajili yako.

Tena elfu wataanguka mkono wako wa kushoto na kumi elfu mkono wako wa kulia lakini haitakukaribia wewe.

Bwana atakulinda kuingia kwako na kutoka kwako.

Umeketishwa Mkono wa kuume wa Mungu Baba katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo Yesu juu sana kuliko falme, mamlaka, usultani, nguvu na kila jina litajwalo si katika ulimwengu huu tu lakini katika ule ujao pia. Unaogopaje kile ambacho umeketishwa juu sana kuliko? Uhai wako umefichwa katika Kristo ndani ya Mungu sasa huko ulikofichwa shetani anakufikiaje?

Mungu wa amani atamseta shetani upesi chini ya miguu yako usikubali akuzingue kwenye ndoto.

Msete upesi pasipo kuchelewa chini ya miguu yako.

Umepewa amri ya kukanyaga ng’e nyoka na nguvu #ZOOOOTE za shetani wala #HAKUNA kitakachoweza kukudhuru ikiwa ni pamoja na hila zake dhidi yako kwenye ndoto.

Hata kama amefanikiwa kupanda kitu maishani mwako kwa njia ya ndoto usiogope maana kila pando asilolipanda Baba wa mbinguni litang’olewa.

Aise utakanyaga simba na nyoka, mwanasimba na joka utawaseta chini ya miguu yako.

Ukiota unakimbizwa na nyoka au na simba huo ni uwongo anaokupandia adui.

Wewe hukimbizwi aise!

Wewe unakimbiza.

Acha kuamini ndoto kuliko unavyoamini Neno la Mungu. Hatuongozwi na ndoto tunaongozwa na Neno la Mungu.

Kila ndoto itapimwa na neno na ikipingana na neno hiyo ni ngome adui anatafuta kuijenga ndani yako.

Angusha hilo wazo na hiyo dhana inayotafuta kujiinua dhidi yako katika ndoto.

Aise una mamlaka ya ajabu katika Kristo.

Acha kuamini ndoto.

Amini neno na pangua kwa neno kila ujinga wa adui unaokuja dhidi yako katika ndoto.

*SHETANI ASIKUZOEE!!!*

*AMAAAAAAAA!*

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...