Sadaka ni nini nini?
Sadaka ni kitendo la rohoni kwanza kwani tunatoa kwa imani. Kumbuka imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17). Imani ni kuwa na uhakika na mambo yatarajiayo (Waebrania 11:1). Kwa hiyo ili uwe na uhakika katika utoaji sadaka, lazima uwe na neno linalohusu sadaka ili Mungu akisema nawe jinsi ya kutoa sadaka uweze kusikia.
Kama huna neno la Kristo juu ya sadaka, huwezi kusikia Mungu akisema nawe jinsi ya kumtolea. Biblia imetoa maelekezo jinsi ya kutoa sadaka hivyo ni vigumu kutolea Mungu sawa sawa na mapenzi yake kama huna hufahamu maandiko yanasema nini juu ya sadaka. Kumbuka usiende mbele za Bwana mikono mitupu (Kumbukumbu 16:16) na pia mtolee Mungu kadri alivyokubariki (Kumbukumbu 16:10).
Kinachofanya sadaka yako iwe sadaka ni imani yako kwa Mungu. “Kwa imani Habili alimtolea dhabihu iliyo bora kuliko Kaini (Waebrania 11:4). Unaposikia neno la Mungu juu ya sadaka linatakiwa likupe uhakika juu ya maelekezo ya Mungu jinsi gani umtolee sadaka. Ukishakuwa na uhakika ndipo unaweka katika matendo kwani imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:26).
Ili uwezi kumpendezesha Mungu katika utoaji wako lazima utoe kwa imani. Maandiko yanatuambia “pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu” (Waebrania 11:6). Usitoe sadaka kidini au kidhehebu ila toa sadaka kwa imani. Hivyo soma sana biblia juu ya sadaka kwani ukishajenga imani jinsi ya kumtolea Mungu huhitaji mtu kukuhimiza kutoa.
Kuna uhusiano kati ya moyo wako na sadaka yako. Mungu akitaka kuujua moyo wako, anaangalia utoaji wako. Maandiko yanasema weka hazina yako mbinguni kwani hazina yako ilipo ndipo moyo wako upo (Matayo 6:20—21). Kitu kikubwa ambacho Mungu anataka siyo sadaka yako ila moyo wako kwanza. Moyo wako ukiwa kwake na sadaka yako itakuwa kwake.
Hivyo kitu cha msingi kabisa ni kujitoa maisha yako kwa Mungu na kumruhusu Yesu Kristo atawale maisha yako. Sadaka yako mbele za Mungu haina maana kama hujautoa moyo wako kwa Mungu. Maandiko yanasema “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA” (Methali 15:8).
Kwa hiyo sadaka ya kwanza ya kumtolea Mungu ni roho na ya pili utoe mwili wako kama dhabihu kwake. Yesu alitupenda na kujitoa kama sadaka na dhabihu kwa Mungu (Waefeso 5:2). Vivyo hivyo yatupasa nasi tuitoe miili yetu kwa Mungu kwani ndio dhabihu iliyo hai (Warumi 12:1).
Hivyo kitu cha msingi zaidi ambacho kanisa inatakiwa ihimize ni watu kuacha njia zao mbaya na kumrudia Mungu ndipo watu wafundishwe juu ya sadaka. Tutengeneze kwanza maisha yetu na Mungu ndipo tutoe sadaka. Yesu anasema “basi ukileta sadaka yako mbele ya madhabahu, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iacha sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako” (Matayo 5:23—24).
Moja ya kazi za Roho Mtakatifu ni kutuongoza (Warumi 8:14). Hivyo inapofika kwenye utoaji wa sadaka, Roho Mtakatifu atakuongoza wapi pa kutoa na jinsi ya kutoa. Moja ya vitu sadaka inaachilia ni wewe kukubalika kwa Mungu (Walawi 19:5). Lakini Mungu hakukubali kwa sababu tu umetoa sadaka ila kwa sababu umetoa sawasawa na maelekezo aliyokupa. Ndio maana ni muhimu sana kujua wakati Mungu anaongea na wewe.
Sadaka haipelekwi mahali popote ila pale ambapo kuna jina lake au uwepo wa Mungu (Kumbukumbu 12:11). Maandiko yanatutahadharisha kutoa sadaka mahali popote (Kumbukumbu 12:13) ila tupeleke mahali Mungu amepachagua. “Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni [makao yake], elekezeni nyuso zenu [hapo], nawe uende [huko]; pelekeni [huko] sadaka zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo (Kumbukumbu 12:5—6).
Hivyo inapofika kwenye suala la utoaji sadaka, Mungu lazima akupe maelekezo ya wapi pa kutoa na jinsi ya kutoa. Muhimu zaidi hakikisha jina lake lipo hapo. Usipeleke sadaka yako mahali ambapo jina lake halipo. Usitoe sadaka kwa sehemu kwa sababu umeona kila mtu anapeleka hapo.
Pia sadaka inatakiwa iwe siri yako wewe na Mungu. Yesu anasema utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume (Matayo 6:3). Dini zingine zinaweka mfumo wa utoaji ambao siyo haupo kwenye maandiko. Ukiona unatoa kiasi kikubwa kwa sababu ya mfumo dini yako imeweka, haumtolei Mungu kibiblia ila unatoa kidini. Unatakiwa utoea jinsi Mungu alivyokubariki na kadri Roho Mtakatifu anavyokuongoza.
Anayetakiwa kujua sadaka yako ni Mungu. Kitu ambacho Mungu anaangalia katika sadaka siyo kiasi unatoa ila imani yako. Unaweza kutoa kiasi kikubwa na Mungu asiikubali sadaka yako na mwingine akatoa kiasi kidogo lakini Mungu akaipokea. Mjane alitoa kiasi kidogo lakini sadaka yake ilikuwa kubwa kuliko zote (Marko 12:41—44).
Mtu haamui jinsi ya kutoa sadaka wala dini/kanisa haiamui jinsi watu watoe sadaka. Mungu ndiye anatoa maelekezo jinsi ya kumtolea. Malekezo haya ni binafsi kwani watu wamebarikiwa tofauti. Kanisa inapoweka kiasi cha utoaji kwa kila mtu, hiyo haipo kwenye biblia. Unaweza kusema “kipindi cha Musa walikuwa wanaambiwa watoe nini na nini.”
Kipindi cha Musa watu waliishi chini ya sheria ila sisi tunaishi kwa imani (Warumi 1:17) kwani sheria imeandikwa katika mioyo yetu (Waebrania 10:16). Kumbuka Yesu Kristo ndiye Kuhani Mkuu wetu na “kila kuhani mkuu huwekwa ilia toe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima naye awe na kitu cha kutoa. Kama angekuwa juu ya nchi asingekuwa kuhani; maana wako watoao sadaka kama iagizavyo sheria” (Waebrania 8:3,4).
Lakini maandiko yanatuambia Yesu ni mjumbe wa agano lililo bora zaidi kwani kama agano la kale lisingekuwa na mapungufu, kusingekuwa na nafasi ya agano jipya (Waebrania 8:6,7). Hivyo sheria ya kutoa sadaka ipo pale pale ila tofauti ni kwamba sisi tunatoa kwa imani. Ndo maana lazima uwe unasoma agano la kale kwa jicho la agano jipya.
Hivyo jenga imani yako juu ya utoaji sadaka ili utoe kadri ya maelekezo Mungu anakupa. Kufuata maelekezo ya Mungu katika utoaji sadaka ni muhimu sana kwani unaweza kutoa sadaka na Mungu akaikataa (Mwanzo 4:5).
Watu wengine wanatoa hera kanisa badala ya kutoa sadaka kwa Mungu. Mungu hahitaji hera yako kwani kila kitu ni mali yake (Zaburi 24:1). Hivyo usitoe sadaka kwa sababu tu umehimizwa na mhubiri au kanisa ila toa kwa sababu umepata maagizo kutoka ya utoaji kwa Mungu. Mungu anaweza kumtumia mhubiri kukupa maelekezo jinsi ya kutoa lakini hakikisha kuwa yanaendana na neno lake.
Mungu hawezi kukupa ujumbe nje ya neno lake. Hivyo ukiona mhubiri anakupa maelekezo ya utoaji sadaka ambao haupo kwenye biblia hiyo sauti ya Mungu. Kuna watumishi wanakuambia toa kiasi fulani ili Mungu afungue milango ya baraka na usipotoa huwezi kubarikiwa. Lakini maandiko yanasema tayari tumebarikiwa na baraka zote za rohoni (Waefeso 1:3).
Ndio maana ni muhimu neno la Kristo likae ndani yako katika hekima yote (Wakolosai 3:16) ili wewe mwenyewe uweze kusikia sauti ya Mungu. Kuna watumishi wanaweka mifumo ya kukusanya hera kinyume na neno la Mungu.
Kuna sadaka za aina nyingi. Mfano sadaka ya hiari, nadhiri, zaka, malimbuko, mbegu, na zingine ila leo tuangalie sadaka za aina mbili:
1. SADAKA YA NADHIRI: Nadhiri ni sadaka ambayo unamuahidi Mungu kwa kinywa chako (Kumbukumbu 23:23). Kwa mfano unaweza kumwambia Mungu “Mungu ukinifanikisha katika biashara yangu, nitakutolea hiki na hiki.” Sadaka ya namna hii inaitwa “nadhiri.” Sadaka ya nadhiri ni sadaka ambayo inafunga nafsi yako (Hesabu 30:2).
Ukiweka nadhiri kwa Bwana hakikisha umeiondoa ili kuondoa kifungo cha nafsi yako (Walawi 27:2). Unapoweka nadhiri kwa BWANA tayari inakuwa sheria ambayo unatakiwa uifuate sawasawa na jinsi hiyo sheria ilivyo (Hesabu 6:21). Hivyo huwezi kuweka nadhiri katika kanisa A halafu ukaenda kuitoa kanisa B.
Maandiko yanatuambia “Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuindoa, kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako” (Kumbukumbu 23:21). Hivyo ukiweka nadhiri Roho Mtakatifu atakukumbusha.
Kama Roho Mtakatifu akikukumbusha juu ya nadhiri ambayo umeiweka wewe ukapuuza au ukashindwa kusikia, atakuja kukudai kama dhambi na maandiko yanatuambia mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Hivyo usiweke nadhiri kama njia ya kumtaka Mungu afanye kitu kama maisha yako halafu hutoi. Weka nadhiri kwa sababu unamwamini Mungu wako kuwa anaweza kukufanikisha katika jambo lolote na usisahau kuiondoa nadhiri yako kwani nadhiri inafunga nafsi yako.
2. SADAKA YA ZAKA: Hii siyo sadaka ya hiari. Maandiko yanatuambia kuwa zaka ni ya BWANA. Zaka siyo sadaka ambayo wewe unamtolea Mungu. Zaka ni mali ya BWANA ambayo ipo mikononi mwako. Maandiko yanasema mwanadamu anaweza kumuibia Mungu (Malaki 3:8). Huwezi kuiba kitu ambacho ni chako. Ile kwamba unaweza kuiba, maana yake siyo chako.
Hivyo 10% ni ya BWANA. Mungu ametoa maelekezo kuwa peleka zaka katika “nyumba ya Bwana” (Malaki 3:10. Kumbuka “zaka ni ya BWANA. “Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; ni takatifu kwa BWANA” (Walawi 27:30). Hivyo usitoe zaka na fikra ya “naenda kumtolea Mungu” bali “nampa Mungu vilivyo vyake.” Yesu alisema “mpeni Mungu yaliyo ya Mungu” (Marko 12:17).
Watu wengi huwa wanapata shida “kuamua” wapi pa kupeleka zaka. Zaka huamui wapi pa kuipeleka ila unaipeleka kwenye “nyumba ya Bwana.” Watu wengine huwa wanauliza “nikitoa zaka kwa yatima na wajane ni vibaya?” Kumbukumbu 26:12—14 inatoa jibu. Hakikisha umeelewa kitu Mungu anasema katika mistari hii. Ukiona wewe ndiwe unaamua pa kupeleka zaka, unamuibia Mungu.
Hesabu 18:21 inatuambia “Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israel kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania.” Walawi hawakuwa na urithi katika Israel ila Mungu ndio alikuwa urithi wao (Hesabu 18:20). Kwa hiyo zaka ndio ilikuwa urithi wao (Hesabu 18:26). Hivyo unaweza kumpatia zaka mlawi kwani zako ni ya Mungu na Mungu ndio urithi wao.
Je natumia njia gani kuamua jinsi ya kumtolea Mungu? Ukitaka kujua kama unavyotoa ni sawa na mapenzi ya Mungu au la jiulize swali hili: Ukiwa unaenda kutoa sadaka yako ghafla Yesu akatokea karibu na kitunga cha sadaka na macho yake yapo kwenye mkono wako, je bado utakuwa na ujasiri wa kutoa kile ulichokuwa unaenda kumtolea?
Kama ujasiri utapotea na utatamani uongeze, basi hautoi sadaka kwa imani. Hivyo rudi kwenye maandiko mpaka upate uhakika ili uweze kutoa sawasawa na mapenzi yake. Sadaka ambayo unaitoa na Mungu haipokei umepoteza hera. Hivyo kabla ya kutoa sadaka, kuwa na uhakika umepata maelekezo yote na kuwa Mungu ameipokea sadaka yako.
Sehemu ya pili tutaangalia baadhi ya sababu za kutoa sadaka. Kama Mungu hajapokea sadaka yako, sababu ya wewe kutoa sadaka inakuwa haipo. Hivyo kile ambacho sadaka inatakiwa iachilie katika ulimwengu wa roho juu maisha yako hupati. Lakini je unajuaje kama sadaka yako imekubalika mbele za Mungu au haijakubalika? Itaendelea…
“Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, na mashinikizo yako yatafurika divai mpya” (Methali 3:9—10).
No comments:
Post a Comment