Saturday, 6 October 2018

MUNGU WETU NI MOTO ULAO


“Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ule ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inavyompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji, kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao” #Waebrania 12:28-29
Nakusalimu mpendwa wangu katika jina la Yesu Kristo aliye hai.
Mwana wa Mungu, ijumaa ya leo ni siku njema ambayo tumepata neema tena tukautafute uso wa Mungu. Kama utakuwa na nafasi ungana nami tukautafute uso wa Mungu kwa maombi ya kufunga kwa masaa 12 kuanzia asbh hadi jioni. Kwa kadri tunavyojizoeza kufanya hivyo ndivyo Bwana anavyotuwezesha kuvuka hatua moja hadi nyingi. “Ujizoeze kupata utauwa.” #1Timotheo 4:7. Haya ni mambo tunayopaswa kufanya mazoezi ya rohoni.
Dunia ya leo mpendwa wangu wangu ni dunia ambayo imebadilika sana. Ni dunia ambayo imekuwa na ukisasa wa mambo mengi. Na watu wakisikia baadhi ya mambo yaliyofanyika miaka mingi sana iliyopita si rahisi sana wengi wetu kukubaliana nayo au kuyaamini. Ndiyo maana kwa sababu ya ukisasa huo tumejikuta tukimuwekea Mungu mipaka. Mfano ni rahisi sana kizazi cha leo kudharau Maandiko Matakatifu katika kizazi chetu tukifikiri kwamba yamepitwa na wakati.
Mwana wa Mungu naomba ujue kuwa ukweli huwa haubadiliki. Na Bwana Yesu ndiye kweli. Hawezi kubadilika. Ni kweli kwamba tunaishi katika zama za agano jipya. Ndugu zetu waliishi katika enzi za agano la kale nasi tunaishi katika agano jipya. Mungu huyu pamoja na maagano haya mawili kubadilika bado BWANA hajabadilika. Kuthibitisha hilo mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaandika kuwa ‘Yesu Kristo ni yeye yule jana na leo na hata milele’ #Waebrania 13:8
Katika dhana ya Mungu kutokubadilika, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaandika dhana ambayo hata katika agano la kale kwamba Mungu wetu tunayemuabudu ni moto ulao. “Kwa kuwa BWANA Mungu wenu ni moto ulao, Mungu mwenye wivu” #Kumb. 4:24. Musa aliyekuwa na uzoefu wa kukutana na Mungu kwa njia ya moto anasema Mungu wetu ni moto ulao. Siku ya kwanza anakutana na Mungu alimuona Mungu kwa njia ya moto ulokuwa ukiwaka kwenye kijiti pasipo kuteketea. Na kwa maeneo mengi sana Musa alimuona Mungu akiwaongoza wana wa Israeli kwa njia ya nguzo ya moto. Musa alikuwa na uzoefu mkubwa wa kumwona Mungu kwa njia ya moto. Na ndiye anasema Mungu wetu ni moto ulao. Mungu huyu huyu ambaye Musa alikuwa na uzoefu wa kumwona kwa njia ya moto na hata akasema Mungu wetu ni moto ulao, ndiye huyo huyo mwandishi wa kitabu cha Waebrania anasema Mungu wetu ni moto ulao. Mungu hajabadilika mwana wa Mungu.
Sasa ngoja tujifunze tabia mbili tatu za moto ukoje. Tukijua tabia za Moto tutaelewa huyu Mungu tunayemuabudu. Katika maandiko moto huwakilisha vitu mbalimbali ktk ulimwengu wa rohoni. Lakini tujifunze tabia chache leo.
MOTO NI HATARI SANA
Mwana wa Mungu moto kwenye maisha yetu unafaida nyingi sana. Tunaweza kupikia, tunawezafanyia hiki na kile. Lakini moto ni hatari. Tusipozitumia kanuni za moto, hakika moto ni hatari. Moto unaweza kuua. Mwaka 2012 nilishuhudia watoto wawili wakifariki maeneo ya kibaha na hakuna kitu kilipona kwenye nyumba ile kwa sababu watoto walicheza na moto. Walikiuka kanuni za moto. Watoto hawa walikuwa wamefungiwa ndani ya nyumba ili wasiende kucheza na wazazi wao wakawa wameenda kazini. Watoto wale wakaanza kuchezea mitungi ya gesi na kuwasha jiko. Moto ulipolipuka Uliunguza kila kitu ndani ya nyumba ile na watoto walikutwa ni majibu.
Tukikiuka kanuni za moto mpendwa wangu, moto ni hatari mno. Tukikiuka kanuni za Mungu wetu hakika tutaangamia. Mungu wetu ni moto ulao ndugu. Ukikiuka kanuni zake jiandae kuangamia. Wako watu walikiuka kanuni za Mungu na moto wa Mungu ukashuka na kuangamiza. “Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao.” #Hesabu 11:1-3
MOTO HUTAKASA
Moto huwa unasafisha vitu. Yamkini umepata kusikia dhahabu husafishwa kwenye moto. Huwa napenda sana kutakaswa kwa moto wa Mungu. Maana moto wa Mungu unapotaka huondoa makandokando yote ndani ya mtu. Ila lazima ujiandae ili Mungu anapofanya oparesheni yake ujue. Wajua majaribu huwa kama moto mwana wa Mungu. husafisha imani zetu na kutufanya tumtumaini Mungu.
Moto wa Mungu huashiria nguvu na uwepo wa Mungu katikati yetu. Moto wa Mungu ni silaha nzuri sana ya ulinzi kwetu. Maandiko yanadhihirisha wazi tunapotembea na Mungu kwa mahusiano mazuri yeye hutugeuza sisi kuwa miali ya moto (#Waebrania 1:7). Lakini pia hutuzungushia ukuta wa moto kutulinda dhidi ya adui.
Sikiliza ndugu yangu, Mungu wetu ni moto ulao. Hata leo hajabadilika. Mungu wetu anaweza kabisa kuangamiza maadui zako kwa moto. Aweza kabisa kuwawashia moto maadui zako na kuwaangamiza. Yakobo na Yohana walimwomba Bwana Yesu waagize moto kutoka mbinguni ili kuwaangamiza watu wa kijiji cha Samaria kwa kuwa walikataa kumopkea Bwana Yesu!(Luka 9:54. Moto wa Mungu waweza kutumika katika ulinzi wetu. Utumie moto wa Mungu lakini hakikisha unasimama katika kanuni za moto usije kukuangamiza. Mungu wetu ni moto ulao.

Mwenye masikio na asikie na Mungu aliye hai akubariki.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nawe mwana wa Mungu na ikiwa umebarikiwa basi share ujumbe huu kwa mwingine naye abarikiwe
“YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, YAWEZEKANA KWA MUNGU” #LUKA 18:27
Kwa maombezi, unataka kupokea uponyaji au kufunguliwa kwenye kifungo chochote kile, ushauri au unatamani ujitoe kikamilifu kumtumikia MUNGU na UNATAKA KUMPOKEA BWANA YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO NA AKUSAMEHE DHAMBI ABADILISHE MAISHA YAKO NA TABIA MBAYA ZILIZOKUSHINDA basi wasiliana nasi kwa msaada wa Roho Mtakatifu tukusaidie +255 758 443 873. Ukipiga simu isipopokelewa tafadhali acha sms

Image may contain: fire and night

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...