Wednesday, 24 October 2018

MAOMBI: KUJAZWA NA ROHO MTAKATIFU


"Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na
Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza
kuwakabidhi kazi hii" #MATENDO 6:3
Nakusalimu mpendwa wangu katika jina la Yesu Kristo aliye hai.
Ahimidimiwe Mungu aketiye mahala pa juu patakatifu kwenye kiti chake cha enzi na ambaye anajishughulisha sana na kazi yake hapa duniani. Na ninamshukuru sana Mungu wetu huyu ambaye leo ametupa nafasi tena ya siku ya 3 ya maombi yetu kwa wiki hii. Ninaamini kuna hatua unapiga ndani yako hata kama unaona mabadiliko ni ya taratibu.
Asante sana wewe ambaye umeendelea kuungana nasi katika maombi haya ya kufunga kila ijumaa hadi jumapili. Asante wewe uliyeungana nasi kwa siku zote 3 au siku kadhaa kutokana na neema ya nafasi uliyoipata. Wewe ambaye hukupata nafasi ya kuomba nasi wiki hii usijisikie vibaya. Ungana nasi wiki ijayo. Mahala popote ulipo endelea kuungana nasi kufunga na kuomba kwa kila ijumaa hadi jumapili lakini pia kila siku kupata kujifunza Neno la Mungu na kuomba. Bwana Yesu anasema "Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga" #Mathayo 17:21. Kuna mambo mengine mpendwa lazima tuyashughulikie magotini tukiwa tumejidhabihu kwa kufunga.
Jumapili ya leo kama ambavyo tumekuwa tukifanya pamoja na maombi yako binafsi mengine, ni siku nzuri ya kumwomba Bwana akujaze na Roho Mtakatifu.
Wanafunzi wa Kanisa la mwanzo walivyokuwa na bidii ya kumtafuta Mungu nyakati fulani kulijaa manung'uniko kuhusu huduma ya wajane hasa wa kiyunani ambao walikuwa hawapewi huduma inavyostahili. Ndipo mitume wakawaambia wanafunzi wachaguliwe watu waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima! Miongoni mwa wanafunzi 7 walioteuliwa alikuemo Stefano na Filipo. Hawa ni kati ya watumishi ambao wanaonekana kwa mbele baada ya kuteuliwa wakifanya kazi ya Mungu na kudhihirisha kujawa kwao na Roho Mtakatifu.
Stefano ni mtu ninayempenda sana. Kwa muda mfupi sana wa utumishi wake unaoonyeshwa kwenye Biblia alidhihirisha matendo makuu ya Mungu ktk kumtumikia kwa utukufu. "Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu". Wakuu wa makuhani walivyojaribu kumkabili maandiko yanasema "hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye" #Matendo 6:8-10. Oooh haleluya! Kwanini usitamani kujazwa na huyu Roho Mtakatifu kila wakati?
Mtumishi Filipo oooh naye usiseme! Aliziba vinywa vya wachawi. Ishara na miujiza ilifanyika kwa mikono yake. Maandiko yanasema kwa ajili ya huduma ya Filipo kwamba "Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule." #Matendo 8:7-8
Nakusihi sana mwana wa Mungu huu ni wakati wa kumtumikia Mungu ktk hali ya ujazo wa Roho wake Mtakatifu. Bila kujazwa na Roho Mtakatifu kila wakati kazi ya Mungu ni ngumu mno. Ngumu kwa sababu tunataka tutumie akili zetu na ufahamu wetu wa darasani badala ya Mungu mwenyewe kutupa neema ya ufunuo na maono na kujazwa na Roho wake Mtakatifu.
Sasa chukua hatua ya kujiombea ujazwe na Roho Mtakatifu. Hakuna fomula katika kujazwa ndugu nakuomba chukua hatua ya kuomba. Ahadi ya Bwana Yesu ni kwamba atatujaza tukimwomba. "Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?" #Luka 11:13
Kwa kadri ya neema ya Mungu juu ya mtu kila mmoja huwa ana neema yake ya kufurika kujazwa na Roho Mtakatifu. Nimeona watu wengine ukigusa tu kuwaombea Roho hushuka juu yao na kuwajaza nao huanza kunena kwa lugha nyingine. Wengine kufurika kwao huchukua muda. Kwa hiyo omba, omba, omba na kuomba hadi uone udhihirisho wa ujazo na endelea kujazwa na kujazwa na kujazwa.
Mungu aliye hai akubariki sana
Ubarikiwe.
YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, YAWEZEKANA KWA MUNGU #LUKA 18:27
Share ujumbe huu kwa wengine kama umependezwa nao ili na wao wabarikiwe.

Image may contain: bird and outdoor

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...