Monday, 24 September 2018

TOBA YA KWELI

 TOBA YA KWELI NI KUZINGATIA KUACHA DHAMBI TOKA MOYONI MWAKO
Bwana Yesu atukuzwe shujaa …
Imeandikwa;

Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; ” Luka 15:17-18
* Toba halisi ni ile ambayo mwamini amezingatia moyoni mwake kuacha dhambi pasipo kujihesabia haki.
Andiko hilo hapo juu,linatuonesha jinsi gani huyu ndugu aliyepotea alipozingatia moyoni mwake kugeuka kutoka katika hali ya uharibifu na kumuelekea baba yake kwa toba.
KUZINGATIA MOYONI.
Ni kugeuka kwa moyo kutoka katika dhambi kwa kuichukia dhambi na kuelekea katika njia safi pasipo kujihesabia haki.
Mtu yeyote atakaye ichukia dhambi,kisha mtu huyo akamuomba Bwana,hakika atasaidiwa atoke katika hiyo dhambi.Vifungo vya dhambi vinamuachia mtu aliyetubia kwa kuchukia dhambi.
Mfano wa kuzingatia moyoni kwa habari ya dhambi;
• Mwamini aweza kuwa amekamatwa na roho ya uzinzi,yaani kila akijaribu kujinasua katika roho hiyo hujikuta akidondoka katika uzinzi ule ule. Sasa anapoenda mbele za uso wa Bwana kwa toba,yampasa aamue kutoka moyoni kuichukia hali hiyo. Maana akiichukia hali hiyo basi ni dhahili kabisa ataepukana na njia zote zinazomuingiza katika uzinzi.
Ila mtu huyo asipozingatia kuichukia dhambi,basi hujikuta AKIIKUMBATIA DHAMBI huku akiitubia. Yaani mfano;
Alizini jana,kisha leo anatubu ila akimaliza kutubu tu,utakuta amekwisha panga kwenda kuzini tena akitegemea kesho atatubu!
• Au mfano,utakuta alizini jana leo anatubu,ila yule yule aliyezini naye bado amemuweka moyoni mwake,akiwasiliana naye na kukutana naye mara kwa mara katika mazingira hatarishi. Mtu wa namna hii HAJAZINGATIA MOYONI MWAKE KUACHA DHAMBI.
Dawa yake,ukiona upo katika kukamatwa na uzinzi,wewe futa mawasiliano na huyo mtu anayekufanya uzini naye. Au hata kama kuna mtu anakushawishi mambo mabaya basi futa mahusiano naye,uiponye roho yako. Maana haiwezekani ukatubu dhambi hiyo,kisha unakwenda kuambatana na yule mwenye kuisababisha.
• Kutubu ni kuzingatia kuacha dhambi kutoka moyoni mwako.
Katika andiko letu la msingi lililopo hapo juu,tunamuona kijana aliyekuwa amepotea katika dhambi ya anasa na kutapanya mali zake zote. Biblia inatuambia kwamba kijana huyu aliamua kutoka moyoni mwake kugeuka moja kwa moja kutoka katika dhambi na kumuelekea Mungu.
Labda ngoja nikupe kisa kamili kilivyokuwa,yamkini utazidi kunielewa;
Kulikuwa na vijana wawili wa baba mmoja ( Luka 15:11-32 ) ambapo kijana mdogo alihitaji apewe mali zake kama ilivyoandikwa, Sasa kwa kifupi mfano wa watatu hawa ( baba,na wana wawili ) wanaweza kulinganishwa na SHINA na MATAWI. ( yaani baba yao ni kama shina,na wale wana wawili ni kama matawi.)
Hivyo,
Tawi moja dogo linaomba liachanishwe na shina ili likawe na maisha mengine binafsi. ” yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Luka 15:12
Ukweli ni kwamba,ikiwa tawi lolote litakatwa na kuachanishwa na shina basi ujue litaonekana na ubichi ule ule lakini kwa muda tu. Baada ya muda si mrefu litanyauka na kufa.
• kumbe tawi haliwezi kuishi lenyewe ni lazima lishikamanishwe na shina.
Ndiposa nikasoma;
Yoh. 15:5,
Kwamba pasipo Mungu,hatuwezi neno lolote.
* Sisi wenyewe hatuwezi kufanya lolote pasipo Mungu.
Maana sisi ni kama matawi,tunahitaji kushikamanishwa na shina.
* nje ya shina kuna mauti.
Tazama habari za Adamu na Hawa walipotoka nje ya shina( Mungu) mauti ikaingia.
Lakini jambo mmoja ninalolipenda ni hili;
• Unapokuwa nje ya shina sababu ya dhambi,Bwana anakutizamia urudi kwake kwa toba halisi. Naye hukusikia kutoka katika shida yako.
Imeandikwa;
* Zab. 118:5
– katika shida yangu nalimuita Bwana,Bwana akanijibu,akaniweka panapo nafasi.
Sasa unisikilize kwa makini;
Mwana mpotevu ( Luka 15:11-32) alikuwa na jina la baba yake. Yaani jina lake la kwanza la kwake, la pili ni la baba yake, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mambo ya nyakati;
” ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. ” 1 Nyakati 7:14
Huyu mwana mpotevu alikuwa ni mtu wa baba yake,aliyeitwa kwa jina lake. Kama vile sisi tuliomkiri Bwana Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wetu,sisi ni watu wake Mungu,tulioitwa kwa jina lake.
Anasema ikiwa kama;
* Tutajinyenyekesha,
* Tutaomba,
* Tutatafuta uso wa Bwana, na
* KUZIACHA NJIA MBAYA
Bwana atatusamehe na kutuponya.
Ilo neno ” kuziacha njia mbaya” ni KUTUBU KWA KUZINGATIA KUACHA DHAMBI KUTOKA MOYONI. Ndipo Bwana atatusamehe,kwa lugha nyingine nje ya hayo bado hatujasamehewa.
Kijana ( mwana mpotevu) alilijua hilo,akaamua kuziacha njia mbaya ili apatane na baba yake. Lakini ” alipozingatia “
Shida ya siku ya leo ipo hivi;
Tunatubu sana pasipo KUZINGATIA KUACHA DHAMBI badala yake tunatubu tukiwa tumezikumbatia dhambi,sasa tutasamehewa vipi?
Utakuta mtu anatubia dhambi fulani,huku kashapanga aifanye tena kisha atubu mara nyingine! Hii ni mbaya sana.
Laiti kama tungejua ya kwamba maisha halisi ya kumpenda Bwana Mungu yapo katika toba ya kweli ya kuzingatia kuacha dhambi,basi tungemaanisha katika eneo hilo la TOBA.Upo upendeleo wa ajabu pale mtu mmoja aliyemaanisha kuacha dhambi kisha akatubu.
Mfano;
Mwana mpotevu aliporejea kwa baba yake,baba yake akamuona tangia mbali na kisha akamuandalia sherehe,akamvisha na pete,na viatu. Vitu ambavyo hata hakumuomba baba yake amfanyie,lakini alifanyiwa sababu ya toba tu. Nasi tumepewa ahadi ya uponyaji kupitia TOBA,Imeandikwa;
” Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, ” Zab.103:3
Najua jambo moja kwamba,sisi ni wakosefu sana,lakini pindi unapoanguka,inuka mara moja kwa toba ya kweli. Chukia dhambi ndugu,na utaponywa na huo ugonjwa pia utapewa na kibali cha ajabu kama vile kwa yule mwana mpotevu aliporudi kwa babaye.

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...