Sunday, 16 September 2018

MUNGU WA UPENDO



 
Shalom watu wa Mungu;
Leo napenda tukajifunze maana halisi ya neno upendo. Sisi vijana tunatumia sana neno upendo. Love….
I love you!
Biblia katika kitabu cha Marko12:29-31 inasema upendo ni “amri ya kwanza”. Katika kitabu cha Mathayo 22:36-40 biblia inasema upendo ni “amri kuu”. Tunaona upendo ni kitu cha msingi sana katika maisha yetu ya ukristo.
Upendo?
Biblia inasema “upendo ni Mungu” 1Yoh.4:8b; 16. Biblia inaendelea kusema katika upendo Mungu anakaa ndani yetu nasi ndani yake. Mungu anakaa ndani yetu katika Roho mtakatifu (1Yoh.3:24).
Point: Kuwa na upendo ndani yako ni kuwa na Mungu ndani yako.
Mungu ni mtakatifu; hivyo aliye na Mungu ndani yake naye ni mtakatifu. Upendo hutuongoza katika mema yote.
Neno la Mungu linasema; 1Yoh.3:18 tusipende kwa ulimi wala kwa neno, bali kwa tendo na kweli. Tusipende kwa midomo; kwamba unamtangazia mtu kuwa unampenda; unatongoza! bali mwenye upendo wa dhati anaonesha katika matendo.
Vijana wengi wamepotea kwa kudhania kitofauti matendo yanayoashiria upendo. Wengine wamedhania uzinzi; lakini hapo wameangukia katika kifo au dhambi. Biblia inasema tena, 2Petro2:13-14 kuna watu ambao wasiokoma kutenda dhambi, wenye macho yajaayo uzinzi, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani… wana wa laana!
Kumbe wapo ambao wanadhani wanapenda kumbe wanatamani tu; wana wa laana! hao ni hatari kwa karamu yenu ya upendo. Wanatamani zinaa na anasa zote; hawakufai kwa kuwa hao watakutenganisha na Mungu wako, yaani watauondoa upendo ndani yako. Haleluya!
Upendo ni kutenda matendo mema. Biblia inasema tupatapo nafasi tuwatendee mema watu wote, Galatia 6:9-10. Tena Neno la Mungu linasema, utawezaje kumpenda Mungu usiyemwona wakati unamchukia ndugu yako unayeishi naye?
Biblia inasema Marko12:31 mpende Bwana Mungu wako; 1.kwa moyo wako wote, 2.kwa akili zako zote na 3.kwa nguvu zako zote. Sehemu ingine Yesu anasema nilipokuwa mgonjwa hamkuja kuniona; nilipokuwa na kiu hamkuninyesha maji; nilipokuwa na njaa hamkunilisha… Mlivyokuwa mnawatendea wale ndugu ndivyo mlinitendea.
Point: ili kumpenda Mungu; kwa moyo wote, kwa akili zote na kwa nguvu zote hatuna budi kufanya hivyo kwa ndugu zetu tunaoishi nao.
Luk10:30-37 tunakuta mfano alioutoa Bwana Yesu; mtu mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Yeriko kwenda Yerusalem aliangukia mikononi mwa wanyang’anyi, vibaka, majambazi… Wakamnyanganya kila kitu hata nguo; walimpiga sana wakamtupa akiwa mahututi karibu kufa.
Alipita kuhani, akamwangalia akampuuza; akafuata mlawi akamwona akampuuza lakini alipita msamaria akamwona akamhurumia. Akamsaidia kwa moyo wake wote, kwa akili zake zote na kwa nguvu sake zote. Msamaria huyo alikuwa na upendo ndani yake; alikuwa na Mungu ndani yake, alikuwa na roho mtakatifu.
Tujitahidi wapendwa kuwa na upendo ndani yetu, kuwa na Mungu ili tuishi katika misingi imara ya wokovu. Mungu awabariki sana.

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...