Monday, 16 July 2018

MOTO NI MKUU!!


“Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” #Luka 3:15-17
Nakusalimu mwana wa Mungu katika jina la Yesu Kristo aliye hai.
Namshukuru Mungu mwema ambaye ameendelea kuwa pamoja nasi siku njema ya leo kwamba tukapate neema ya nafasi kumtumikia Mungu. Asante wewe uliyekuwa pamoja nasi katika maombi ya kufunga jana. Asante pia kwa ajili yako wewe ambaye utakuwa pamoja nasi leo kuungana pamoja nasi.
Jana nilikupa kwa sehemu ufunuo wa ujumbe wa kinabii kwamba Mungu wetu ni moto ulao. Nikakuonyesha kwa sehemu ndogo kwamba ili tumjue Mungu kama moto ulao, lazima tujifunze tabia za moto zikoje. Tukaona kwamba moto ni hatari. Tusipotumia kanuni vizuri za moto hakika tutaangamia. Vivyo hivyo tusipotumia kanuni vizuri za kumtumikia Mungu hakika tutaangamia. Tukaangalia tabia ya pili ya moto kwamba moto una nguvu. Vivyo vivyo tukaona kwa moto wa Mungu juu yetu tunapata nguvu ya kumtumikia Mungu.
Ngoja niongezee kidogo kwenye huu ujumbe wa jana kwamba moto ni mkuu. Asili ya moto siku zote ni mkuu. Hakuna moto baridi hata kama moto huo ni mdogo kwa kiwango gani. Moto ni moto. Moto sio wa kuchezea hata kama ni mdogo kwa kiwango gani. Hata kama moto utakuwa mdogo sana hakika unaweza kuunguza na kuleta madhara makubwa. Kwa hyo usifanye mchezo na moto eti kwa sababu ni mdogo.
Sikiza ndugu yangu, Mungu wetu ni Mungu mkuu kwa asili na kwa tabia yake. Chochote anachokifanya huwa anakifanya kwa ukamilifu wake mkuu. Yeye mwenyewe pale msalabani alituokoa kikamilifu kabisa. Hakubakisha kitu. Damu yake iliyomwakiga pale msalabani ilitoa wokovu mkuu kwa kila amwaminiye Yesu.
Huyu Mungu ni mvumilivu sana kwa kila mwanadamu. Usione ujinga unaoufanya halafu unadhani kana kwamba Mungu amekaa kimya. Ni kwa sababu tu Yeye ni mvumilivu kwako. Yeye alituokoa kwa ukamilifu kabisa pale msalabani. Damu yake ilimaliza ukombozi kamili pale msalabani. Ghadhabu yake ikiamua kushuka juu yako kwa sababu ya uovu unaoufanya itashuka kama moto mkuu na hautabaki salama. lakini Bwana amekuwa akikuvumilia tu.
Hakuna kitu kilichobaki katika kutukomboa pale msalabani. Ukombozi wake umekamilika. Mungu ameonyesha pendo lake kuu kwetu pale msalabani hajabakisha kitu chochote katika ukombozi wetu. Mtume Paulo anasema ‘Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu’ #Wafilipi 1:6. Kazi njema ya ukombozi aliyoianzisha pale msalabani hata akakuokoa mpendwa wangu hakika ataikamilisha. Upendo wake ni mkuu mno kwako. Usijiangalie katika hali ya kawaida ya kimwili unayoipitia na changamoto zake.
Pendo la Mungu ndani yetu ni kuu. Amemimina pendo lake ndani yetu kwa Roho wake Mtakatifu. Moto ambao Roho Mtakatifu ameuwasha ndani yetu ni mkuu mno. Haijalishi dunia imekuwa baridi kwa kiwango gani lakini moto ambao Roho wa Mungu ameuwasha ndani yetu hakika ni mkuu utayeyusha kila aina ya uchungu na ubaridi wa dunia unaotukabili. Upendo wa Mungu ni mkuu mno ndani yetu
Kama ambavyo upendo wake ni mkuu ndani yetu vivyo hivyo hukumu zake ni kweli na ni hakika na hukumu zake ni kuu. Mungu ni Mungu mwenye haki, Mwana wa Mungu nikuhakikishie usifikiri Mungu kwa pendo lake kuu juu yetu anaweza kuiangalia dhambi ndani yetu na iache hivi hivi. Chochote au yeyote aliye kinyume na mwana wake mpendwa Yesu Kristo basi yu kinyume na Mungu Baba. Dhambi yeyote inayosumbua ndani yetu inatufanya tuwe kinyume na Mungu wetu aliye hai. Na Mungu atashughulika na dhambi hiyo, atashughulika nawe ipasavyo. Ghadhabu ya Mungu dhidi ya dhambi hiyo ni kuu kuliko moto. Mungu ni mkuu mpendwa wangu hatuwezi kumdharau na kujichafua na dhambi. Atatushughulikia ipasavyo. Ghadhabu yake hailinganishwi na ukuu wa moto. Moto wa Mungu utawaangamiza waovu lakini huwatakasa wenye haki kila siku.
Kwa hiyo jmosi ya leo pamoja na maombi yako mpendwa hebu jichunguze binafsi uone kama liko eneo ambalo dhambi imekutesa chukua hatua ya kukaa magotini kwenye toba. Ghadhabu ya Mungu haitakuacha hivi hivi kama umeachilia mlango wa dhambi ndani yako. Usiache pia kuniombea neema ya Mungu inifunike ktk kazi ya Mungu.
Mwenye masikio na asikie na Mungu aliye hai akubariki.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nawe mwana wa Mungu na ikiwa umebarikiwa basi share ujumbe huu kwa mwingine naye abarikiwe
“YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, YAWEZEKANA KWA MUNGU” #LUKA 18:27
Kwa maombezi, unataka kupokea uponyaji au kufunguliwa kwenye kifungo chochote kile, ushauri au unatamani ujitoe kikamilifu kumtumikia MUNGU na UNATAKA KUMPOKEA BWANA YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO NA AKUSAMEHE DHAMBI ABADILISHE MAISHA YAKO NA TABIA MBAYA ZILIZOKUSHINDA basi wasiliana nasi kwa msaada wa Roho Mtakatifu tukusaidie +255 758 443 873. Ukipiga simu isipopokelewa tafadhali acha sms

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...