Sunday, 22 July 2018
BIBLIA INASEMA NINI KUHUSU KUNENA KWA LUGHA?
BIBILIA INASEMA NINI KUHUSU KUNENA KWA LUGHA?*
Mpendwa wangu, ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai.
Leo natamani tupite katika maandiko ili tuone kile ambacho maandiko yanasema kuhusu kunena kwa lugha.
Yapo mafundisho ambayo yanasema sio lazima mwamini anene kwa lugha.
Yapo ambayo yanasema kuwa ni lazima mwamini anene kwa lugha.
Ila mimi natamani tuangalie kile ambacho maandiko yanasema kuhusu kunena kwa lugha.
*Marko 16: 15 – 18.*
*15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. 17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.*
Wakati Yesu anawapa agizo wanafunzi Wake wakahubiri Injili kwa kila kiumbe, aliwaambia kuwa aaminiye na kubatizwa ataokoka alafu anawaambia ishara ambazo zitafuatana na hao waaminio.
Mojawapo ya hizo ishara ni kwamba yeye aaminiye atasema au atanena kwa lugha mpya.
Kwa hiyo hapa tunaona kabisa kuwa kunena kwa lugha ni moja ya ishara za waaminio.
Paulo katika Waraka wake kwa Wakorintho anaandika:
*I Korintho 14: 22.*
*22Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini lakini kuhutubu si kwa ajili yao wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio.*
Wanafunzi wa Yesu walipojazwa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste walinena kwa lugha mpya kama ambavyo Roho wa Mungu aliwajalia.
*Matendo 2: 4.*
*4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.*
Hapa ni wazi kuwa wote walijazwa Roho Mtakatifu na wakaanza kunena kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka.
Petro alivyokuwa anahubiri nyumbani kwa Kornelio, waliyokuwa wanamsikiliza nao walijazwa Roho Mtakatifu wakaanza kunena kwa lugha mpya.
*Matendo 10: 44 – 47.*
*44Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. 45Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. 46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, 47Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?*
Petro na wale waiyoambatana pamoja naye walijuaje kuwa mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu?
Waliwasikia wakisema kwa lugha mpya au kunena kwa lugha.
Kwa hiyo kule kunena kwa lugha ndo ishara ya nje mojawapo inayodhihirisha kuwa mtu amejazwa Roho Mtakatifu.
Hakuna mahali popote kwenye maandiko ambapo inasema au inaashiria kuwa kuna mtu alishawahi kujazwa Roho Mtakatifu alafu haikuambatana na ishara ya kunena kwa lugha.
Paulo alikuwa ni mtu ambaye ananena sana kwa lugha.
*I Korintho 14: 18.*
*18Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote;*
Pia Paulo Mtume aliwasemesha Wakorintho kuhusu kutowazuia watu kunena kwa lugha.
*I Korintho 14: 39.*
*39Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha.*
Zipo faida lukuki za kunena kwa lugha lakini mimi leo natamani kusema kidogo kuhusu faida ya kunena kwa lugha katika maombi.
*Warumi 8: 26, 27.*
*26Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. 27 Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.*
Kila mmoja wetu bila ya kujali tupo katika hatua gani ya kukua kiroho anao udhaifu katika kuomba.
Mara nyingi huwa hatujui tuombe nini na hata tungejua tuombe nini hatujui jinsi ya kuomba itupasavyo.
Katika hali hiyo Mungu anatusaidia kwa Roho Wake Mtakatifu na huyo Roho Mtakatifu anatusaidia kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
Tafsiri ya NENO ya bibilia ya Kiswahili inasema kuwa Roho Mtakatifu hutusaidia kwa kutuombea kwa uchungu usiyoweza kutamkika.
Kwenye tafsiri ya Kiswahili ya Habari Njema bibilia inasema Roho Mtakatifu hutuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usiyoweza kuelezeka.
Huko kuugua kusikoweza kutamkwa ninaamini ndo hiyo lugha tunayojaliwa na Roho Mtakatifu.
Mungu kupitia Nabii Sefania alilizungumzia hili:
*Sefania 3: 9.*
*9Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja.*
Ninaamini hii lugha iliyo safi ambayo anaizungumzia hapa ni lugha ya maombi tunayojaliwa na Roho Mtakatifu.
Hii lugha tunajaliwa ili tuweze kuliitia Jina la Bwana au kwa maneno mengine tuombe.
Paulo katika kuwaandikia Wakorintho alisema:
*I Korintho 14: 2.*
*2Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.*
Tunapoomba kwa lugha tunayojaliwa na Roho Mtakatifu, huwa tunakuwa tunazungumza moja kwa moja na Mungu na katika roho zetu tunazungumza au tunaomba mambo ya siri.
Hilo neno *“siri”* kwenye tafsiri za kiingereza linatumika neno *“mysteries”* ambalo neno sahihi zaidi la Kiswahili ni neno *“Mafumbo.”*
Ndo sasa utaelewa alikuwa ana maana gani aliposema hatujui kuomba itupasavyo maana vitu vingine ni mafumbo ya kiroho.
Inawezekana umeomba kwa kila namna unayojua kuomba juu ya jambo fulani na huoni upenyo wala kusogea katika hilo sio kwa sababu unachokiomba sio sahihi bali ni jambo ambalo lipo kama fumbo na hakuna namna hata Mungu angekuelezea unaweza kulielewa.
Roho Mtakatifu ndo hutusaidia katika maswala kama hayo kwa kutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa na ninaamini huko kuugua kusikoweza kutamkwa ndo kunena kwa lugha kwenyewe na sababu kuu ya kunena kwa lugha katika maombi ni kuweza kuomba ipasavyo katika maswala ambayo hatuna uelewa wa ndani wa kutosha kwa akili zetu.
Kwa mfano unaweza ukasikia mzigo wa kuomba lakini hujui hata uombe nini au uombee nini au hata wakati mwingine huo mzigo unakuja kabisa na jina au sura ya mtu lakini hujui shida ni nini na unatakiwa kuomba nini au kuombea nini.
Hapa sasa ndipo utaona faida ya kujazwa na Roho Mtakatifu kwa ishara ya kunena kwa lugha maana unaanza tu kuliombea hili jambo au kuomba sawa na mzigo uliyowekwa ndani yako kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Paulo Mtume anasema:
*I Korintho 14: 14, 15.*
*14Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. 15 Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.*
Kumbe tukiomba kwa lugha ambayo tunajaliwa na Roho Mtakatifu, roho zetu kwa msaada wa Roho Mtakatifu huomba lakini akili zetu hazina matunda au kwa maneno mengine hazielewi kinachoendelea wala kinachoombewa.
Sasa haimaanishi kila wakati tuombe kwa roho tu lakini msisitizo wangu ni kwamba kuna kiwango na vina vya maombi huwezi kuvifika kama huneni kwa lugha au hujaweza kuomba kwa lugha ambayo Roho Mtakatifu anamjalia kila mwamini.
Paulo akizungumza na Waefeso alisema:
*Waefeso 6: 18.*
*18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;*
Paulo anasisitiza kuwa katika sala zetu zote na maombi tukisali kila wakati katika Roho.
Nilivyomwelea hapa ni kwamba kila ninaposali au ninapoomba kama sijapata pia fursa ya kusali na kuomba katika Roho au kwa msaada wa Roho Mtakatifu nakuwa sijaomba ipasavyo katika jambo husika.
Mtume Yuda katika Waraka wake anasema:
*Yuda 1: 20.*
*20 Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,*
Hapa panasisitizwa tena kuhusu kuomba katika Roho Mtakatifu na tunapozungumzia kuomba katika Roho Mtakatifu huwezi ukatenganisha na kunena kwa lugha.
Ujazo wa Roho Mtakatifu kwa ishara ya kunena kwa lugha ni haki ya kila aaminiye.
Badala ya kutafuta sababu kwanini huneni kwa lugha tamani na tafuta kujazwa Roho Mtakatifu kwa ishara ya kunena kwa lugha maana itakupeleka kwenye kiwango kingine kabisa cha maombi.
Mungu akubariki sana.
Uwe na wakati mwema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...
-
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...
-
Bwana Yesu asifiwe… Imeandikwa ; “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; “Y...
-
Ni miaka mingi nimekuwa nikijiuliza swali hili, nitawezaje kumpenda Mungu kwa moyo wangu wote, kwa akili zangu zote na kwa nguvu zangu zote...

No comments:
Post a Comment