Thursday, 9 November 2017

Aina za Maombi:
Image result for MAOMBI NI NINI
Maombi yamegawanyika katika aina kadhaa. Tutaziangalia hapa chini kama ifuatavyo.
1.Maombi ya Vita
Tunajua kabisa tuko vitani katika maisha yetu. Na peke yetu hatuwezi kupigana vita hii. Kwa hiyo ni lazima tumshirikishe Mungu vita hii. 1Tim 6:12 – Piga vita, 2Kor10:4- Silaha za vita vyetu.
Tunapokuwa kwenye maombi haya ya vita, tunatakiwa kuelewa mambo yafuatayo:
a). Tuwajue vizuri maadui zetu tunaopigana nao.
b). Tuzijue silaha ambazo Mungu ametupatia.
c). Tujifunze vizuri namna ya kutumia silaha zetu, vinginevyo silaha hizo zitageuka kutudhuru sisi. (Ukitupa bomu la mkono vibaya litakulipukia wewe mwenyewe).
d). Tuzijue vizuri silaha anazotumia adui yetu.
Maombi haya ya vita ni maombi ya wakati wote wa uhai wa binadamu, kwa kuwa vita hii katika ulimwengu wa roho hukoma pale tu mtu anapokufa.
2. Maombi ya Toba
Image result for MAOMBI NI NINI
Maombi haya ya toba yanatakiwa yafanywe kwa makini sana. Yohana 9:31 inasema Mungu hawasikii wenye dhambi. Maombi ya toba ni maombi ya kujutia yale tuliyoyafanya ambayo hayakumpendeza Mungu. Lengo la maombi haya ni kuungama makosa tunayoyajua na tusiyoyajua na kuamua kutokuyarudia tena na kuomba Mugu atuepushe kufanya makosa tusiyoyajua.
Yohana 8:11, …Usitende dhambi tena!. Pia Yohana 5:14. Katika maandiko haya kuna kielelezo cha toba. Mwanamke alikamwatwa kwenye zinaa na akaletwa kwa Yesu akishitakiwa. Walitaka kumpiga kwa mawe lakini Yesu alimsaidia. Neno linasema Yesu aliinama akawa anaandika chini, japo haikuelezwa alikuwa anaandika nini. Lakini wanatheolojia wanasema, yawezekana alikuwa anaziorodhesha dhambi za kila mmoja aliyekuwa pale, hao ambao walitaka kumpiga kwa mawe yule mwanamke. Wote walipojiona wakakimbia. Na yule mwanamke akabaki peke yake na Yesu. Na ndipo alipoambiwa maneno hayo: Usitende dhambi tena!
Tunamwona pia mtu aliyekuwa amelala kwa mika 38, katika birika la Bethzatha [Yohana 5:2-9]. Kulala kwa miaka 38 inaonyesha mtu huyo anayo sifa ya uvumilivu, ambayo wengi wetu tunashindwa. Tunaamua kuhama hama kutafuta hiki na kile. Yesu alimkuta yule mtu akiwa amelala na akamuuliza, Unataka kuwa mzima? Nadhani jibu lake lilikuwa jepesi, tena rahisi: Ndiyo! Lakini ona anavyozunguka: ‘Mimi sina mtu wa kunitia birikani, ninapotaka kuingia mwingine hunitangulia’ Alikuwa hajaulizwa kama ana mtu wa kumtia birikani wala hakuulizwa kwa nini haingii kwenye birika, hakuulizwa kwa nini haponi. Hayo maswali ndiyo yangejibiwa kama alivyojibu. Lakini yeye aliulizwa, ‘Unataka kuwa mzima?’
Hili ni tatizo la watu wengi wanapokwenda kwenye maombi. Badala ya kufanya toba ya kweli, wanabaki kuzunguka. Mwanzo 3:11-12, Ni nani aliyekwambia kuwa uko uchi? (Nimejiona); Je, umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? (Ndiyo).  Lakini hapa Adamu alijibu, ‘Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda nikala’.
Swali, kwenye Mwanzo 3:13, Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Ni nini hili ulilofanya?. ( angejibu Nimekula tunda au nimempelekea Adamu au nimemkosesha Adamu). Lakini yeye Hawa alijibu ‘Nyoka amenidanganya nikala’. Unaona hapa?
Mungu hakumuuliza nyoka swali bali alimpa adhabu tu. Kwa nini hakumuuliza? Mungu hakumuuliza nyoka kwa sababu Nyoka alikuwa amefanya kazi yake. Yeye huitwa Mjaribu, Mwongo, Mtega mitego nk. Hiyo ndiyo kazi ambayo shetani anafanya na amemwacha aendelee kufanya hivyo. Ndiyo maana Yesu akasema tuangalie mtu asitudangaye. Mathayo 24:4.
Katika maombi ya toba ni vema kuangalia sana tunavyoungama mbele za Mungu. Kuna uwezekano mkubwa tusitake kutubu makosa yetu bali tukaanza kutafuta yule aliyetukosesha. Toba sahihi ni  ile ambayo mtu hujutia makosa yake yeye mwenyewe na kujiona ni yeye ndiye anahusika kwa makosa hayo. Hali hii ndiyo huleta toba yenye maana.
3. Maombi ya Kujilinda.
 Image result for MAOMBI NI NINI
Efeso 6:13- Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana…... Wakati tunaposema ‘silaha’ inaonekana kama ni silaha za kushambulia. Lakini hebu nikuonyeshe kitu hapa:
Mungu anasema ‘vaeni silaha zote’: Kweli viunoni, Dirii ya haki kifuani, Utayari kwenye miguu, Ngao ya Imani, Chapeo ya wokovu, Upanga wa Roho (Neno) na Sala zote na Maombi. Silaha zilizotajwa hapo ni za kujilinda isipokuwa mbili tu ndizo za kushambulia adui, ambazo ni Upanga wa Roho na Sala zote na Mombi. Ndiyo maana nikasema ziko silaha za kujilinda:-
Kweli viunoni – Tunapaswa kuwa wakweli hata kama inatugharimu maisha yetu. Ndiyo maana Yohana 8:32 inasema hivi, Mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru. Kuwekwa huru maana yake ni kutokuogopa chochote. Wakati mwingine tumeogopa wanadamu tukaanguka kwenye mtego. Mithali 29:25, Kuwaogopa wanadamu kunaleta mtego. Kwa kule kusema, kweli viunoni ana maana kweli ifungwe kiunoni kama unavyofungwa mkanda, isitoke. Ni baada ya kufungwa kweli viunoni ndipo tukakuwa wajasiri kama simba. Mithali 28:1, Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
Dirii ya Haki Kifuani – Hili linajieleza lenyewe.
Utayari miguuni – Kwa sababu miguu ndiyo inayotembea. Hapa imetumiwa kuwakilisha utendaji. Ni wangapi mpaka sasa hawajafikiwa na Injili? Nani atawafikia? Ni yule aliye tayari kwa kutoa Muda wake, Fedha zake na hata maisha yake.
Ngao ya Imani – Siku zote adui yetu hutupa mishale, tena ya moto. Imani peke yake ndiyo itatusaidia tusidhurike na mishale hiyo anayoitupa. Imani ni muhimu sana na inawindwa ili tunyang’anywe.
Wakati wa misukosuko baharini kwenye mtumbwi Yesu aliwauliza wanafunzi wake, ‘Imani yenu iko wapi’?. Luka 18:18, Atakapokuja mwana wa Adamu ataikuta Imani? Yakobo 2:14-17, Imani bila matendo imekufa. Watu wengi wanaodai kuwa wanayo Imani, lakini matendo ya ile Imani hayaonekani, maana yake ni kwamba Imani hiyo imekufa.
Chapeo ya Wokovu – Chapeo ni kofia ngumu. Mwendesha piki piki hutakiwa kuvaa chapeo [Helmet] ambayo inaweza kumsaidia wakati wowote akianguka ili asiumie kichwa. Kichwani kuna vitu vingi, ikiwa ni pamoja na Ubongo. Ubongo ndio kiungo cha muhimu sana katika mwili wa binadamu. Ni sawa na kompyuta. Kumbukumbu zote ziko hapo kwenye ubongo. Hivyo panatakiwa kulindwa ili pawe salama. Na hapo ndipo palipo na uwanja wa vita kwa kuwa kabla mtu hajatenda dhambi yoyote: huona au husikia, hunusa au huonja kisha ubongo unatafakari. Na baada ya kutafakari nafsi ya mtu ikiruhusu lile lililotafakariwa likateremka moyoni, hapo ndipo moyo hufanya uamuzi wa ama kukataa au kukubali lile lililotafakariwa kisha mhusika huchukua hatua.
Sasa basi tumeona silaha hizo za kujikinga, tumalizie na silaha za Kushambulia.
Upanga wa Roho (Neno) – Naziita silaha za kushambulia kwa sababu ndizo tunatumia kumshambulia adui yetu. Tunampinga kwa neno. Yakobo 4:7, Basi mtiini Mungu, mpingeni shetani naye atawakimbia. Wako watu wengi ambao hujaribu kumpinga shetani kabla hawajamtii Mungu. Hiyo ni hatari. Kumbuka wana wa Skewa walijaribu kulitaja jina la Yesu mapepo yakawararuwa. Mdo 19:14 Kuna wakati tunapaswa kumshambulia adui akiwa mbali, kama vile kwa kutumia silaha aina ya mzinga. Hatutakiwi kumngoja hadi atuvamie ndipo tumpige.
Sala zote na Maombi – Hizo pia ni silaha za kushambulia. Maana tunatakiwa kuomba sawa na Neno la Mungu linavyosema. 1Yohana 5:14-15, Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake ya kuwa tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake atusikia vema. Na kama tukijua kwamba atusikia tuombacho chote, twajua ya kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.
Tukiomba twapasa kuamini, kwa maana imeandikwa tukisitasita Mungu hawi na furaha na sisi. Pia katika Ebrania 11:6, Lakini pasipo Imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
4. Maombi ya mahitaji ya kiroho na kimwili
Katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na uhitaji wa vitu mbali mbali: Chakula, mavazi, malazi, uponyaji nk. Neno la Mungu linatuelekeza pia kuomba juu ya mambo kama haya. Luka 6:9-15. Natumaini hili halihitaji maelezo mengi kwa kuwa linajitosheleza.
Baada ya kuwa tumeona aina mbali mbali za maombi sasa tuangalie Makundi makuu Mawili ya maombi.
Maombi, katika ujumla wake, yamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni MAOMBI YASIYO NA UKOMO na MAOMBI YENYE UKOMO. Kwa maneno mengine ni maombi ya kudumu na maombi yasiyo ya kudumu.
Maombi yasiyo na Ukomo:
Image result for MAOMBI NI NINI
Katika 1Thes 5:17 tunapata maneno haya: Ombeni bila kukoma. Andiko hili ni kwa ajili ya maombi ambayo hayana mwisho. Mwisho wa maombi haya ni pale tutakapofika nyumbani kwa Baba yetu. Katika Luka 18:1 imeandikwa, Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumuomba Mungu siku zote wala wakikate tamaa. Neno linasema tuombe bila kukoma. Neno linasema pia tuombe Mungu siku zote wala tusikate tamaa.
Kama nilivyosema mahali fulani kuwa tunapigana vita, na kamwe shetani hataacha vita mpaka atakapotupwa motoni. Hii ina maana siku zote tutaendelea kuwa na vita, na kama ndivyo hivyo lazima Tudumu katika Maombi. Maombi ya kudumu ni jumla ya maombi yote yanayohusu mambo ya rohoni: Toba, Vita, Kujilinda kwa kuwa tungali duniani, twakaa na watu mbali mbali huku safari ya mbinguni ikiwa inaendelea. Pia maombi kama vile kuombea amani ya miili yetu na nchi zetu ni maombi ya kudumu.
1Yohana 3:3- Kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa. Kujitakasa ni kitu endelevu. Mara nyingi twamkosea Mungu wetu kwa mawazo, maneno na matendo. Ndiyo maana baada ya kumjua Mungu vizuri Daudi alisema katika Zab 19:14 kwamba Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu na mwokozi wangu. Tunatakiwa kuyatafakari wakati wote maneno haya aliyoyasema Daudi mtumishi wa Mungu.
Maombi yenye Ukomo:
Image result for MAOMBI NI NINI
Katika Mathayo 21:22 tunapata maneno haya, Na yo yote mtakayoomba katika sala mkiamini, mtapoke. Mtu anayeomba kitu halafu akakipokea ni wazi kwamba hawezi kuendelea kukiomba tena. Mifano: mtu anayeomba Mungu ili apate mke/mume, baada ya kuwa ameoa/ameolewa hawezi kuendelea kuombea tena hitaji hilo. Mtu anapoomba kwa ajili ya kupata uponyaji, akiponywa hawezi kuendelea kuomba maana ameshapokea alichokuwa anahitaji. Kwa ujumla ni kwamba mtu anapokuwa anaombea hitaji fulani akilipokea huo ndio unakuwa mwisho wa ombi hilo.
Sasa, kwa kuangalia haraka haraka, ni rashisi mtu kusema kwamba Biblia inajipinga, kwa sababu kule inasema tuombe bila kukoma, halafu huku inasema tukiamini tutakuwa tumepokea. Na kama mtu akipokea kinachofuata ni kushukuru! Sasa kama tunatakiwa kushukuru kwa nini tena tuendelee kuomba bila kukoma? Jibu la wasi wasi huu ni hilo kwamba kuna mambo ambayo tunapoomba majibu yake ni dhahiri, na uhitaji huo huishia hapo. Lakini hata kama si dhahiri, yaani bado ni kwa Imani, lakini baada ya muda kitu hicho hudhihirika na hivyo kutokuwepo haja tena ya kuendelea kuombea kitu hicho hicho tena. Maombi yote yanayohusu mambo ya kimwili yako kwenye kundi hili. Kuna wakati tunatakiwa kuacha kuombea jambo fulani la kimwili hata kama hatukupata jibu lake. Maombi pia kama vile uhitaji wa kujazwa na Roho mtakatifu, kufanikiwa katika huduma fulani, nk, nayo yanaingia katika kundi hili.
Jambo jingine la kuzingatia katika maombi yenye ukomo ni kwamba siyo lazima jibu la maombi hayo liwe ni ndio. Kuna uwezekano wa mtu kuomba kitu ili apatiwe lakini Mungu akamwambia hapana! Na hapo ndiyo ukawa mwisho wa maombi ya kitu hicho. Tatizo kubwa ambalo hutokea sehemu hii ni kwamba kuna wakati mwingine watu huomba huku jibu wanalo tayari. Sasa inapokuwa imetokea kinyume na jinsi walivyoomba, ni rahisi sana wao kufikiri kwamba Mungu hajajibu, kwa kuwa walitaka Mungu ajibu kwa njia ambayo wao wanaona inafaa. Lakini kwa kawaida jibu la maombi yoyote linaweza kuwa Ndiyo, Hapana au Subiri. Na lolote katika hilo huwa ndilo ambalo Mungu Baba ameona kuwa linafaa.
Hebu tuangalie mfano mmoja katika 2Kor 12:7-10, Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo, nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Ujumbe huo unajieleza wenyewe. Mtume Paulo aliomba mwiba mtoke. Hilo ndilo lilikuwa ombi lake na aliomba huku akitegemea jibu la ndio, kwa maana alikuwa anateseka. Ndiyo maana aliomba mara tatu: Mara ya kwanza hakuna jibu, akaomba tena mara ya pili, hakuna jibu, akaomba tena mara ya tatu ndipo Mungu akamwambia ‘hapana, kwa kuwa Neema yangu yakutosha’. Na baada ya jibu hilo yeye alifurahia kwa kuwa ndivyo Bwana alivyoona inafaa. Na ndipo baadaye akaja kuelewa sababu ya kutokuondolewa kwa mwiba huo: ili asije akajisifia kwa vile Mungu alivyokuwa akimtumia. Hali hiyo akaifurahia na akakubali matokeo! Na akawa tayari kukubali kubaki na mwiba huo hadi mwisho wa maisha yake. Lakini baada ya kujibiwa vile hakuendelea tena kumuomba Bwana aundoe mwiba huo. Maombi hayo yalifikia ukomo siku ile alipojibiwa.
Mfano mwingine unaofanana na huo unapatika katika kitabu cha Kumb 3:23-28 ambapo Musa mtumishi wa Mungu alimuomba Mungu ili aingie nchi ya Ahadi, [Kaanani] lakini Bwana Mungu alimkatalia.
Kutokana na mifano hiyo miwili tunajifunza kwamba tunapoomba jambo lolote kwa Mungu tunakiwa kukubali matokeo, huku tukijua kwamba kwa kuwa Mungu ni Baba yetu kamwe hawezi kutupatia nyoka badala ya samaki au jiwe badala ya  mkate. Wakati wa kujibiwa ‘hapana’ inawezekana isiwe rahisi kuelewa lakini kwa kuwa tunayemwomba ni Baba yetu ni lazima atatufahamisha kwa nini ameleta jibu la ‘hapana’. Kwa kuwa ikiwa ni ndiyo au hapana, kama ni Mungu ndiye aliyejibu basi lolote kati ya hayo lengo lake ni jema kwetu!
Hayo ndiyo makundi makuu mawili ya maombi. Lakini katika maombi ya kundi lolote ni lazima kushukuru. Kwa yale yasiyo na ukomo ni lazima kushukuru kwa kuwa kila tunapokuwa tumeomba, kwenye hatua fulani, Mungu huwa ameshatenda. Lakini pia twapasa kumshukuru Mungu hata kwa yale ambayo atatenda. Kwa maombi yale yenye ukomo, tukipokea tulichokiomba ni vema tukamshukuru Mungu. Lakini hata kama tumekipokea kwa Imani tu na hakijadhirika kimwili, pia tunatakiwa kushukuru tu. Na shukurani hizi zinatakiwa kuendelea kuwepo hata kwa yale ambayo majibu yake ni ‘hapana’. Hivi ndivyo Biblia inavyosema katika 1Thes 5:18 kwamba Shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.
Dalili moja wapo ya siku za mwisho ni watu kukosa shukurani. 2Tim 3:2. Hebu tupende mkumshukuru Mungu kwa yale anayotutendea na yale atakayotutendea pia. Katika Luka 17:11-19 tunapata habari ya Bwana Yesu alipowaponya wale wakoma kumi (10) lakini ni mmoja tu ndiye aliyerudi kushukuru, mpaka Yesu mwenyewe akashangaa. Yule aliyerudi kushukuru aliambiwa na Yesu kwamba Imani yake 

Imemuokoa.  Yaani tayari alishashugulikiwa na rohoni pia. Shukurani kwa Mungu ni jambo la mumihu sana kila tunapokuwa tumepeleka maombi mbele za Mungu
Shetani, ambaye ni adui yetu, anajua maandiko. Ndiyo maana alipomwendea Yesu ili amjaribu alitumia maandiko, akisema ‘imeandikwa..’. Katika siku za mwisho shetani atawafanya watu wasimrudishie Mungu shukurani, wakose kushukuru ama kwa kuwasahaulisha au kwa kuwafumba wasione chochote chema kutoka kwa Mungu. Mtu asiye na shukurani ni rahisi sana kuingiliwa na tabia ya kunung’unika, na manung’uniko si jambo jema mbele za Mungu.
Kwa hiyo katika yote tunayoomba ni lazima tuwe watu wenye kushukuru ili tusiingie katika kundi la watu wenye kutimiza maandiko.

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...