Friday, 4 August 2017

(UTUKUFU WA MSALABA)



Waheshimiwa wapendwa,
Leo tunaadhimisha Utukufu wa Msalaba. Tumshukuru Mungu kwa Upendo huo mkubwa kutufia msalabani na tumwombe tuwe wavumilivu tunapoteseka maishani na atuongezee Imani kwa Kristu ili tupate uzima wa milele.

Umuhimu wa Msalaba

Nawakaribisha tutafakari juu ya Umuhimu wa Msalaba. Tunajua Yesu alikufa msalabani. Basi ingetosha hilo jambo kuandikwa katika Biblia kama matukio mengine aliyofanya Yesu. Kwa nini tunaendelea kuwa na hii ishara ya msalaba katika Kanisa na katika maisha yetu?  Misalaba imetundikwa kila mahali. Je, kuna umuhimu wowote wa kuwa na hii ishara ya msalaba? Kwa hiyo, leo hatuangalii kwa nini Kristu alitufia msalabani (Rej. Mahubiri Siku ya Ijumaa Kuu) bali tunaangalia umuhimu wa kuwa na msalaba.
Kuna sababu nyingi za kuwa na msalaba lakini leo naomba tunagalie sababu tatu tu:
a)      Msalaba ni ishara ya Mapendo
b)      Msalaba ni ishara ya Ushindi
c)      Msalaba ni ishara ya Unyenyekevu

1. Msalaba ni Ishara ya Mapendo

Tunapomwangalia Yesu msalabani tunatambua jinsi Mungu anavyotupenda. Katika msalaba Mungu amedhihirisha kwa ulimwengu mapendo makuu aliyonayo kwa wadhambi na kwa ulimwengu mzima. Tumeachiwa msalaba uwe ishara ya mapendo ya Mungu kwetu. Msalaba na Ekaristi ambavyo ni Sadaka moja vinaonyesha Mapendo ya Mungu kwetu.
Yesu alimwabia Nikodemo: “Mungu Baba aliupenda hivyo ulimwengu hata akamtoa Mwanae wa pekee.” Ukombozi wetu unaanza na Upendo wa Mungu kwetu. Kristu mwenyewe alishasema:
Hakuna upendo ulio mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yn 15:13).
Wanaofunga ndoa hupeana pete “Mwenzangu pokea pete hii, iwe ishara ya mapendo yangu kwako.” Jinsi hiyo, kwa njia ya msalaba Kristu ananiambia mimi na anakwambia wewe “Mwenzagu pokea msalaba huu, uwe ishara ya mapendo yangu kwako.
Kwa hiyo, tunapoangalia msalaba tunaona jinsi Mungu anavyotupenda. Tunamuona Mungu si kama hakimu atakayetuadhibu kwa sababu ya makosa yetu bali Mungu mwenye upendo ambaye anafanya lolote lile ili aweze kumpata mdhambi na kumrudisha kwake; aweze kumrudisha mdhambi katika uhusiano mwema nayeSifurahii kifo cha mtu mwovu bali aache njia yake mbaya akaishi” (Eze 18:23).

Utambuzi huu una umuhimu gani?

i)     Tukitambua kuwa Mungu ni mwenye huruma tunamwendea na uhakika wote atusamehe dhambi zetu kama alivyofanya mtoto mpotevu “Nitaondoka na kurudi kwa Baba”(Lk 15:18) na hivyo tunakiendea kitubio na kusamehewa dhambi zetu na hivyo, tunapona.
ii)  Tunafuata kila anachotufundisha. Tunaamini kuwa alichofundisha Kristu ni kweli na kinafaa kutufikisha mbinguni kwa sababu anatupenda. Hivyo tunaishi kadri ya amri zake bila kulalamika tukikumbuka Mungu alivyotwambia: “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msilikizeni yeye.”
iii)  Tukitambua mapendo ya Mungu kwetu inakuwa sababu ya kuwapenda wezetu
Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu” (1Yn 3:16).
iv)   Tukitambua mapendo yake kwetu, tunavumilia kila mateso tukijua kuwa Mungu ana nia njema na sisi
Mungu hakumuhurumia hata Mwanae wa pekee bali alimtoa kwa ajili yetu. Kama amefanya hivyo je, hatatujalia na mema yote?” (Rum 8:32).

2. Msalaba ni ishara ya Ushindi

Tunapomwangalia Yesu Msalabani tunatambua kuwa “Kuna ushindi katika mateso.” Ili kuweza kuelewa ukweli huu tujiulize swali hili: Kwa nini tunasema ‘Utukufu wa Msalaba’?
Tunasema ‘Utukufu wa msalaba’ kwa sababu ni katika Msalaba Kristu alipata ushindi dhidi ya dhambi na mauti; dhidi ya shetani. Katika safari nzima ya kutukomboa Yesu alikuwa katika mapambano na kishawishi cha kuukimbia msalaba na kuchukua njia rahisi (Rej. Yesu akijaribiwa Mt 4:1-11). Akiwa Gethsemani Kristu alifikiria msalaba na akaogopa
Moyo wangu una huzuni karibu kufaBaba kama inawezekana kikombe hiki kinipite mbali”(Mt.26:38-39).
Kama Yesu asingekubali hiki kikombe; kama asingekubali kufa msalabani tusingekombolewa na yeye asingeingia katika ufukufu.
Lakini “alijinyenyekeza akawa mtii mpaka mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa(alimwingiza katika utukufu)” (Wafilipi 2:8-9).
Kwa hiyo, ni katika msalaba Kristu alipata ushindi wake. Kwa kufa msalabani si kwamba ameshindwa kujitetea bali amekishinda kile kilichokuwa kikimvuta asikubali kufa msalabani.
Kama Musa alivyomwinua nyoka jangwani ndivyo na Mwana wa Mtu atakavyoinuliwa.” Angalia neno ‘Kuinuliwa – kukwezwa, kuwekwa juu.’ Kile alichokuwa ameomba ametimiziwa:
Baba, ile saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza” (Yn 17:1) – “Niimarishe niende msalabani maana ni hapo nitadhihirisha ushindi na upendo wako.

Fundisho

a)      Tukubali kuteseka tunapojiwa na vishawishi

Mara nyingi katika maisha hatutaki kuteseka. Tunahitaji njia rahisi. Kristu ametuonyesha kuwa kama tunataka utukufu,basi tukubali kuteseka. Utukufu hauji kwa ujanja wa kukwepa mateso bali kwa kuvumilia hayo mateso kwa imani. Waswahili wanatwambia:
Mtaka cha uvunguni sharti ainame” Huwezi kushika kilicho chini ya kitanda kama umesimama. Lazima uiname.
Hakuna ‘Taji la Utukufu’ bila ‘Taji la Miiba’”- No crown without cross.
“Hakuna Pasaka bila Ijumaa Kuu”.
Lakini pia kwa msalaba Kristu ametuonyesha kuwa atakayevumilia mateso hatateseka bure kwa sababu
Mchumia juani hulia kuvulini”- Yesu amechumia juani akitundikwa msalabani; sasa analia kivulini anapofurahi kuwa ametimiza alichokuja kukifanya maana alishasema:  “Nitakapoinuliwa juu nitawavutia watu wote kwangu”(Yn 12:32). Hayo yametimia naye anafurahi.
Kwa hiyo, katika maisha tunapopambana na kishawishi fulani lazima tukubali kuteseka, kwa sababu kishawishi kinatuelekeza kwenye njia rahisi inayoonekana kuleta furaha lakini inatupeleka kinyume na mapenzi ya Mungu. Tukifuata mvuto huo, tunaanguka. Lakini tukikubali kujitesa na kujinyima hizo furaha za muda, basi katika hayo mateso tunapata ushindi dhidi ya kishawishi, ushindi dhidi ya dhambi.
Ndiyo maana Kristu anatutahadharisha:
Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele”(Yn 12:25).
Kwa hiyo, msalaba unatuonyesha kuwa kuingia katika utukufu wa mbinguni si lelemama. Ni mapambano. Tukijifanya mayai mayai na kujihurumia tukikubali kila kishawishi tutajipoteza. Lakini tukiwa ‘ngangali’kwa vishawishi tutayaokoa maisha yetu.

b)      Tukubali mateso yanayotokana na imani yetu

Tunapodhurumiwa au tunapolazimika kuteseka kwa sababu ya majukumu tuliyonayo kiimani au katika jumuiya au kanisa, tusilalamike au kuona kuwa tunasumbuka bure. Kama Kristu ameingia katika utukufu kwa njia ya mateso sembuse sisi. Ndiyo maana Mt. Luka anatwambia
Lazima sisi sote tupitie katika taabu nyingi ili kuingia katika ufalme wa Mungu” (Mdo 14:22).
Ifike wakati tuelewe faida ya mateso yetu na tuseme kama Mt Paulo:
Na sasa ninayo furaha juu ya mateso ninayopitia… kwa sababu, kwa mateso haya ninasaidia kutimiliza kile kilichopungua katika mateso ya Kristu kwa ajili ya mwili wake yaani kanisa(Kol.1:24).
Kwa hiyo, tunapokabiliwa na mateso katika maisha na kukaribia kukata tamaa kwa Mungu hatupendi kama walifanya Waisraeli jangwani, basi angalia msalaba

3. Msalaba ni Ishara ya Unyenyekevu

Ukimwangalia Yesu msalabani, kwa macho ya kibinadamu, utaona unyonge, utaona kushindwa. Lakini ni katika unyonge huo, ni katika kushindwa huko amepata ushindi na utukufu. Paulo anatwambia
Kwa wale wanaopotea msalaba ni upuuzi. Lakini kwetu sisi ni nguvu ya Mungu” (1Kor1:18).

Fundisho: Tuishi maisha ya upole na unyenyekevu

Katika mahusiano ndani ya familia, katika ndoa au katika kazi na jumuiya zetu, ukichukua njia ya unyenyekevu na msamaha, utaonekana mpumbavu, mwoga; utaonekana kushindwa au kutokuwa na nguvu “kutokuwa mwanaume.” Lakini, ni katika upole huo tunaweza kuishi vizuri na kila mtu maana
Mungu amevichagua vile ambavyo ulimwengu unaviona ni dhaifu ili aviabishe vyenye nguvu (1Kor1:27-28). Hiyo ndiyo hekima ya kweli.
Ndoa nyingi zimevunjika, mahusiano mengi yamevurugika kwa sababu ya kila mmoja kujifanya mjuaji na kutaka kujionyesha ana nguvu.
Hata kama una nguvu, uwezo, cheo au pesa, unaishi kana kwamba huna vyote hivyo ukifuata mfano wa Kristu ambaye
Kwa asili alikuwa daima Mungu lakini hakuona kule kuwa sawa na Mungu kama ni kitu cha kushikamana nacho kwa nguvu. Akaachilia hayo yote; akajitwalia hali ya mtumwa(Filp 2:6).
Kwa hiyo, tumeachiwa msalaba kama ishara ya unyenyekevu ili kila mara tukiangalia msalaba wa Yesu tukumbuke unyenyekevu wake na hivyo kujitahidi sisi wenyewe kumfuata katika njia hiyo.

Hitimisho

Hivyo, basi tunapomwangalia Yesu msalabani tunatambua mapendo na unyenyekevu wake; na hivyo, tunapata nguvu ya kushindana bila kushindwa mpaka tufike pale yeye alipo katika utukufu wa mbinguni.

No comments:

Post a Comment

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu. Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande m...